Maskini!! Ofisi Ya Kanumba The Great Yafungwa Usiku Wa Manane

Ofisi ya Kampuni ya Kanumba The Great Films illiyopo Sinza Mori Dar imefungwa rasmi huku vitu vikihamishwa usiku.

Inauma sana! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya kusikia habari hii kuwa ile ofisi ya aliyekuwa mwigizaji kinara wa sinema za Kibongo, Steven Charles Kanumba ‘Marehemu Kanumba The Great’ iitwayo Kanumba The Great Films iliyokuwa maeneo ya Sinza-Mori jijini Dar imefungwa rasmi huku vitu vikihamishwa usiku.
 
Tukio hilo la kusikitisha lililoshuhudiwa na wanahabari wetu lilijiri Februari 2, mwaka huu, majira ya saa 1:30 usiku baada ya kutonywa na jirani mmoja anayefanya biashara zake karibu na ofisi hiyo.
 
Shuhuda huyo alidai kwamba mtekelezaji wa zoezi hilo ni mmoja wa watoto wa Mama Kanumba, Flora Mtegoa (jina halikupatikana mara moja) ambaye aliamua kufanya shughuli hiyo usiku ili kukwepa kuonekana.

Marehemu Steven Kanumba akiwa na tuzo za filamu enzi za uhai wake.
“Ninyi Global mnapitwa, mtoto wa Mama Kanumba anahamisha vitu ofisini kwa Kanumba, tayari zoezi limeanza,”  alisema jirani huyo aliyeomba hifadhi ya jina na kuongeza kuwa ofisi hizo zinahamishwa mahali hapo kwa sababu kodi ya jengo hilo imeongezeka kutoka laki mbili za awali na kuwa laki sita kwa mwezi, gharama ambayo inatajwa kumshinda mama huyo.
Wakiendelea kupangua vitu.
Wanahabari wetu walifika eneo la tukio ndani ya dakika sifuri ambapo walishuhudia gari aina ya Toyota Canter likiwa limepaki nje ya ofisi hiyo huku watu wanaodaiwa kuwa  ni wabeba mizigo wakiingia na kutoka ndani ya ofisi hiyo wakiwa na vitu mbalimbali kisha kuviingiza kwenye gari hilo.
Kwa ustadi mkubwa, mapaparazi wetu waliopiga kambi katika eneo hilo walishuhudia masanduku ya vioo yaliyokuwa yakitumika kuwekea CD na DVD za marehemu Kanumba yakipandishwa kwenye gari hilo.
Baada ya zoezi hilo kushika kasi, wanahabari wetu walizama ndani na kujionea hali halisi ambapo walishuhudia chumba kikiwa wazi huku picha za ukutani zikiwa zimeshushwa na kuwekwa pamoja na vitu vingine tayari kwa kupandisha kwenye gari.

...Akiwa kazini enzi za uhai wake.
Hata hivyo, mtu aliyetajwa kuwa mmoja wa watoto wa Mama Kanumba aliwazuia mapaparazi wetu kupiga picha za ndani ya chumba hicho na kujifungia mlango kwa ndani huku wakisitisha zoezi la kupakiza vitu kwenye gari kwa muda wakiwataka mapaparazi waondoke eneo hilo.
 
Akizungumza na waandishi wa habari, mmoja wa wabeba mizigo hao alisema kuwa, walifika eneo hilo na gari lao kwa ajili ya kuhamisha mizigo kutoka ndani ya ofisi hiyo na kuongeza kuwa yeye hakufahamu chochote zaidi ya mhusika mwenyewe ambaye ni mtoto wa Mama Kanumba.

Mama Kanumba alipopigiwa simu na mwandishi wetu alikiri kupandishwa kwa kodi ya ofisi hiyo kwa kiasi kikubwa na kudai kuwa alishindwa kulipa fedha hizo kwa kuwa hapati faida yoyote kutokana na ofisi hiyo zaidi ya hasara.
Gari likiwa maeneo ya Sinza Mori.
“Kwa kweli kodi imekuwa kubwa mno, siwezi kulipa maana tangu mwanangu afariki dunia (Aprili 7, 2012) siku hadi siku kodi imekuwa ikizidi.
“Kipindi Kanumba anafariki dunia kodi ilikuwa laki mbili kwa mwezi, tangu hapo imekuwa ikipanda mara kwa mara mpaka sasa ni laki sita kwa mwezi na wanataka nilipe yote ya mwaka mzima, kusema kweli nimeshindwa.
“Hakuna kikubwa ninachonufaika na kampuni kiasi cha kulipa fedha nyingi kiasi hicho japo nimefanikiwa kutoa filamu mbili tu mpaka sasa.
“Nimeamua kuachana nayo (ofisi) nitafakari sehemu nyingine ya kuendeleza kampuni,” alisema Mama Kanumba.

Kufungwa kwa ofisi ya Kanumba kunakuja ikiwa ni siku chache baada ya kuibuka kwa skendo kuwa ilikuwa imegeuzwa kichaka cha ufuska na baadhi ya wasanii na machangudoa ambao usiku huonekana nje ya ofisi hiyo na wateja wao.
 
Hadi sasa haifahamiki kama ndiyo mwisho wa Kanumba The Great Films au itafunguliwa sehemu nyingine au ndiyo imekufa moja kwa moja japokuwa kuna taarifa kuwa mara baada ya ofisi ya Kanumba kufungwa, kwa sasa ofisi hiyo ina mpangaji mpya.
~Gpl
Maskini!! Ofisi Ya Kanumba The Great Yafungwa Usiku Wa Manane Maskini!! Ofisi Ya Kanumba The Great Yafungwa Usiku Wa Manane Reviewed by habari motto on 10:43 AM Rating: 5
ads 728x90 B
Powered by Blogger.