ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba amesema hatoongea chochote kinachohusu masuala ya uongozi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unatarajia kufanyika Oktoba.
Jaji Warioba alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana katika uzinduzi wa kampeni ya Vuguvugu la Uhuishaji Maadili inayofanywa na chama cha wataalam Mbalimbali wa wakristo(CPT)alipotakiwa kutoa maoni kuhusu mchakato wa uchukuaji fomu za kugombe urais unaoendelea katika Chama Cha Mapinduzi(CCM).
Alisema katika kipindi hiki cha mchakato wa kuelekea katika uchaguzi mkuu sio raisi mtu akaongea jambo la msingi likaeleweka katika jamii.
“Nilisema kwa kipindi hiki nitakaa kimya sitoongea,kwa sababu muda huu ukisema chochote kinahusishwa na uchaguzi mkuu jambo ambalo sitaki linitokee,hata hapa nimekubali mwaliko huu kwa sababu ya ushawishi ha heshima ya rafiki yangu (Profesa Kanywanyi)”alisema Jaji Warioba.
Alisema hakubaliani na baadhi ya watangaza nia wanaojiita waadilifu kwakuwa kuna baadhi yao wanatoa rushwa na wengine wanafuata taratibu za kawaida katika mchakato huo.
Alisema kulingana na misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kila mtanzania anapaswa kuwa mzalendo na mwajibikaji.
Alisema mgongano wa maslahi katika baadhi ya maeneo ni chanzo cha ufisadi kuporomoka kwa maadili mambo ambayo yanaweza kuhatarisha amani ya nchi.
“Viongozi na jamii kwa ujumla wanapaswa waichunge amani iliyopo nchini kwakuwa ikipotea itakuwa aibu kwa Taifa,”alisema Warioba.
Alisema kwa sasa kuna dalili ya ukabila,udini na ubaguzi wa rangi,kikanda na wakichama unaanza kurudi jambo ambalo linachangia kuhatarisha amani na uporomoshaji wa maadili.
Alisema nchi haiwezi kuwa na viongozi wenye maadili endapo jamii inayowazunguka haina maadili.
“Jamii haionyeshi kama inataka viongozi wenye maadili kwakuwa inachangia kuporomosha maadili,hakuna mtu ambaye anaweza akamrekebisha mwenzake katika hili,”alisema Jaji Warioba.
Awali akitoa mada kuhusu suala la uhuishaji maadili Mwnyekiti wa CPT,Profesa Beda Mutagahwya alisema kwa sasa Taifa limekuwa na kashfa mbalimbali zinazohusisha watumishi wa umma na watawala ambao wengi wao hawajachukuliwa hatua zozote za kinidhamu na kisheria.
“Kumekuwa na wimbi la rushwa,uvunjaji wa haki za binadamu bila kuchukuliwa hatua,uvunjaji wa haki za binadamu bila kuchukuliwa yote haya yanaamsha hasira za umma na kutufanya tusema sasa yatosha,”alisema Profesa Mutagahwya.
Alisema kitendo cha kutafsiri kama bahati mbaya ama ajali kazini kwa matukio ya dhuluma na maovu ni kudalilisha Taifa kwakuonekana limekosa umakini.
Alisema kuna umuhimu wa kujenga upya maadili ya Taifa ambayo kwa sasa yameporomoka na kuhatarisha amani na maendeleo ya nchi.
Alisisitiza wahusika wanapaswa kutunga miundo mipya ya utawala,sheria mpya,kuimarisha vyombo vya usalama pamoja na kuunda tume za maadili na taasisi za kuzuia rushwa.
Jaji Warioba: Sitaongea Chochote Kuhusu Uongozi kuelekea Uchaguzi
Reviewed by habari motto
on
6:19 AM
Rating:
Reviewed by habari motto
on
6:19 AM
Rating:
