BADO KUNA MAFICHO YA MABILIONI USWISI
Wakati kukiwa na taarifa zinazothibitisha kuendelea kwa utoroshaji wa fedha kwenda nje ya nchi, imebainika kuwa ni vigumu kumalizwa kwa tatizo hilo kutokana na ukweli kwamba uhai wa baadhi ya benki nchini Uswisi unategemea fedha haramu.
Kadhalika utoroshaji huo unachangiwa na udhaifu wa sheria za kodi na ile ya madini za hapa nchini, ambazo zinatoa mwanya kwa kampuni zinazowekeza katika sekta hiyo kutolipa kodi ipasavyo, badala yake fedha hizo kuhamishiwa nje ya nchi.
Taarifa za hivi karibuni zinasema fedha nyingi zinazopelekwa mafichoni nje ya nchi, nyingi zinatokana na ukwepaji kodi na sehemu kubwa ya fedha hizo zinafichwa katika benki za Uswisi, zikitokea katika sekta ya madini.
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa hivi sasa kuna mvutano katika sekta ya benki nchini Uswisi, unaotokana na msukumo wa baadhi ya wanataaluma kutaka kuwapo kwa uwazi wa kibiashara ili kubaini benki zinazojihusisha na biashara hiyo.
Dk Mark Herkenrath ambaye ni ofisa programu wa taasisi ya Alliance Sud inayojishughulisha harakati za kupinga uwekaji wa fedha haramu nchini Uswisi, alisema miongoni mwa changamoto za kukabiliana na utoroshaji wa fedha kutoka nchi zinazoendelea ni kuwapo kwa benki nchini humo zinategemea biashara ya fedha haramu:
“Utakuta baadhi ya benki za Uswizi hasa zile ndogo na za binafsi zinategemea biashara za fedha haramu na zingependa kuwe na mtiririko wa fedha haramu kutoka nchi zinazoendelea,” alisema Dk Herkenrath na kuongeza: “Siwezi kuzitaja hizo benki kwa kuwa baadhi ninafanya nazo kazi, zitajua tu mimi ndiye niliyetoa siri, lakini pia sheria zetu za kibenki haziruhusu kabisa kutaja majina ya wateja wa benki hata kama ni fedha haramu.”
Alikiri kuwapo kwa mvutano katika sekta ya benki, ambapo baadhi wanataka kuwe na uwazi na wengine wanataka biashara hiyo iendelee kwa sababu ndiyo inawapatia mishahara.
Mwishoni mwa wiki iliyopita uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ulikiri kwamba taasisi hiyo imekuwa ikipoteza mabilioni ya shilingi kutokana na ukwepaji mkubwa wa kodi unaofanywa katika maeneo kadhaa ikiwamo sekta ya madini.
Madini yalitajwa katika taarifa ya Global Financial Integrity, kwamba yanatumia mwanya uliowekwa katika msamaha wa kodi ya mafuta yanayotumika kwenye migodi, kuhamisha fedha na kutolipa kodi nyingine wanazostahili.
TRA wafunguka
Kamishna wa walipakodi wakubwa, Neema Mrema akizungumza na gazeti hili baada ya mkutano wa waandishi wa habari, alisema TRA imekuwa ikipoteza kodi nyingi kwa kutozingatiwa kwa taratibu za uhamishaji wa fedha kwa njia ya ununuzi (Transfer Price).
“Ni kweli mapato mengi yamekuwa yakipotea tangu tulipoingia kwenye sera ya uwekezaji miaka ya 1990. Tuna mifano ya kampuni na wafanyabiashara wanaotumia mbinu hiyo kukwepa kodi, lakini sheria haituruhusu kutaja majina,” alisema na kuongeza: “Siwezi kusema hadi sasa tumepoteza kiasi gani, lakini ni fedha nyingi, hivyo Wizara ya Fedha na ile ya Nishati na Madini zikae mezani na kupitia upya mikataba ya madini”.
Mtafiti wa kodi za kimataifa wa TRA, Allan Moova alisema kuwa upotevu wa kodi katika sekta ya madini unasababishwa na makubaliano ya mikataba ya madini ya tangu awali:
“Tuna matatizo makubwa tangu wakati tunaingia makubaliano ya mikataba ya madini (MDAs), yaliweka hali ambayo hata sheria zikitungwa lazima zitatoa mwanya wa kukwepa kodi. Ndiyo maana unaona kampuni nyingi za madini hazilipi kodi hizo,” alisema Moova.
Msemaji Mkuu wa BoT, Emmanuel Mwero alisema kuwa taasisi yake ndiyo chombo pekee kinachosimamia shughuli za benki na vyombo vingine ambavyo vinajishughulika na fedha, hivyo kina jukumu la kutoa taarifa zinazohusiana na utakatishaji wa fedha haramu zitokanazo na shughuli za vyombo hivyo.
“Sheria inazielekeza benki na taasisi za fedha kutoa taarifa mara tu itakaposhuku kuwa mteja wake au mtu yoyote anapanga kujihusisha na utakatishaji wa fedha haramu kwa namna yoyote ile. Taarifa hii inaweza kutolewa BoT au kwenye chombo mahsusi ‘The Financial Intelligence Unit (FIU),” alisema Mwero katika majibu yake ya maandishi kwa gazeti hili.
Kamati ina jukumu la kuishauri Serikali kuhusu masuala ya upambanaji na upatikanaji wa fedha haramu, ikiwa ni pamoja na utoroshwaji wa fedha haramu kwenda nje.
Aliitaja sheria nyingine inayoipa BoT mamlaka ya udhibiti wa utoroshwaji wa fedha kwenda nje ya nchi kuwa ni ile ya fedha za kigeni (The Foreign Exchange Act) ya 1992.
Alisema katika kutekeleza majukumu yake, FIU hupelekewa taarifa zote na kufanyia uchambuzi wa kina na kwamba wakiridhika kutendeka kwa kosa, taarifa hupelekwa kwenye vyombo vya sheria ili hatua stahiki zichukuliwe.
MWANANCHI
HII NDIYO TUHUMA NYINGINE KWA SERIKALI YA TANZANIA...
Reviewed by habari motto
on
10:00 AM
Rating: