Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kwa mara nyingine ametunukiwa tuzo la kimataifa – zamu hii kwa kuwa mshindi wa Tuzo la Nyota wa Demokrasia Afrika 2014 – Icon of Democracy Award Winner for 2014 in Africa.
Kwa mujibu wa barua aliyoandikiwa Rais Kikwete na kupokelewa Ikulu, Dar Es Salaam, Rais Kikwete amekuwa mshindi wa kwanza, na kwa mbali kabisa, katika mchuano na marais watatu wa Afrika ambao walifikia mwisho mwa mchuano wa kuwania tuzo hilo.
Katika barua hiyo, Mchapishaji na Mhariri Mkuu wa Jarida hilo, Pastor Elvis Iruh, akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Tuzo 2014, amesema kuwa uongozi wa Rais Kikwete umekuwa ni hadithi ya kusifiwa ya mafanikio katika Bara ambako hadithi za namna hiyo siyo nyingi.
Tuzo hilo hutolewa na Jarida la The Voice na mwaka jana mshindi alikuwa ni Rais Bai Koroma wa Sierra Leone ambaye alikuwa ni mshindi wa pili wa Tuzo hiyo ambalo ilitolewa kwa mara ya kwanza kwa Rais wa Kwanza wa Zambia, Mzee Kenneth Kaunda.
Sherehe maalum ya kukabidhi tuzo hiyo imepangwa kufanyika Oktoba 17, mwaka huu, 2014, katika Hoteli ya Van der Valk, iliyoko Almere, Uholanzi.
Miongoni mwa sifa nyingine, Rais Kikwete anatunukiwa Tuzo hiyo kwa sababu ya kuwa msimamizi mzuri na wa kweli wa demokrasia, kuendelea kuhakikisha kuwa amani, utulivu na maendeleo vinaendelea kupatikana katika eneo la Afrika ambalo limepitia vipindi vingi vya migogoro na matatizo.
Aidha, gazeti hilo linasema kuwa Rais Kikwete amekuwa kiongozi wa mfano, kimataifa na kikanda, na linatoa mfano wa mchango wake katika kusuluhisha mgogoro mkubwa wa kisiasa nchini Kenya kufuatia uchaguzi mkuu wa 2007.
Rais Kikwete pia anasifiwa kwa mchango wake katika kusimamia maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbali mbali – kilimo, elimu, miundombinu, maendeleo ya viwanda, utalii na pia mchango wake katika kuendeleza vijana na kutoa nafasi nyingi kwa akinamama kushika nafasi nyingi za uongozi.
Jarida la The Voice pia limempongeza Rais Kikwete kwa kuimarisha Umoja na Muungano wa Tanzania na kutoa nafasi kwa wananchi kujadili na kukubaliana kuhusu Katiba Mpya ya Tanzania. Aprili mwaka huu, Rais Kikwete alitunukiwa tuzo la kuwa kiongozi mwenye mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Afrika kwa mwaka 2013 – The Most Impactful Leader in Africa 2013.
Na Mwandishi Maalum
NA HII NDIYO TUZO YA HESHIMA BARA LA AFRIKA, ALIYOSHINDA RAISI KIKWETE 2014,
Reviewed by habari motto
on
10:25 AM
Rating: