APANDISHWA MAHAKAMANI KWA UGAIDI



Mtuhumiwa namba moja katika kesi ya kujihusisha na vitendo vya ugaidi, Sheikh Farid Ahmed (mbele) akiwa na watuhumiwa wenzake chini ya ulinzi wa askari Magereza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory


Dar es Salaam. Kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Farid Hadi Ahmed (43) na mwenzake Jamal Nooridin Swalehe (38), wameunganishwa na watu wengine 18 wanaoshtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka manne likiwamo la kula njama ya kuingiza watu nchini kushiriki katika vitendo vya ugaidi.
Pia, wanakabiliwa na shitaka la kuwaingiza watu nchini kushiriki katika vitendo vya ugaidi, kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo hivyo.
Mawakili wa Serikali, Peter Njike, Bernard Kongola na George Barasa wakiwasomea hati ya mashtaka hayo yanayowakabili washtakiwa hao walidai kuwa Sheikh Farid ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbuyuni, Zanzibar na Fundi Ujenzi, mkazi wa Koani Zanzibar, Swalehe walijihusisha na makosa hayo ya ugaidi kinyume na Kifungu cha 27(c) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya 2002.
Mbali na Farid na Jamal, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na mashtaka hayo ni Nassoro Hamad, Hassan Bakari, Ahtari Humoud, Mohamed Isihaka, Abdallah Hassan, Hussein Mohamed, Juma Sadala, Said Kassim, Hamis Amour, Abubakar Abdallah, Salum Ali, Salum Amour, Alawi Othuman, Rashid Ally, Amir Hamis, Kassim Salum na Said Shehe.
Walidai kuwa kati ya Januari 2013 na Juni mwaka huu washtakiwa hao kwa pamoja walipanga njama ya kutenda makosa hayo ya kula njama za kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo vya kigaidi.
Njike alidai kuwa katika kipindi hicho na maeneo tofauti nchini, Sheikh Farid aliwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary nchini ili kushiriki kutenda makosa ya ugaidi.
Pia Sheikh Farid anadaiwa kuwa kwa makusudi na akijua, alitoa msaada kwa watu hao wa kutenda vitendo vya kigaidi kinyume cha sheria. Pia anadaiwa kuwa katika kipindi hicho akiwa anajua kuwa Sadick na Farah wametenda makosa ya kigaidi, aliwahifadhi.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine.
Hakimu Hellen Liwa aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 20, mwaka huu na kuamuru washtakiwa kupelekwa rumande kwa sababu mashtaka yanayowakabili ni miongoni mwa mashtaka yasiyo na dhamana.
Baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili, Sheikh Farid alidai mahakamani hapo kuwa anashangazwa na kitendo cha wao kukamatwa Zanzibar na kushtakiwa Tanzania Bara wakati hawana ndugu, baba wala mama katika upande huo wa Jamhuri ya Muungano.
“Tunashangaa kushtakiwa huku Tanganyika wakati Zanzibar ni nchi yenye Mwanasheria Mkuu, Jaji Mkuu na askari watiifu tu na kila kitu,” alisema na kuongeza kuwa wamekamatwa Aprili lakini hadi sasa upelelezi bado haujakamilika na kuhoji ni upelelezi gani huo.

NA MWANANCHI

APANDISHWA MAHAKAMANI KWA UGAIDI APANDISHWA MAHAKAMANI KWA UGAIDI Reviewed by habari motto on 9:39 AM Rating: 5
ads 728x90 B
Powered by Blogger.