Mwili wa mpiga debe huyo baada ya kifo chake |
DENI la Sh 2,000 limetosha kumaliza uhai wa mpiga debe maarufu wa stendi ya mabasi yaendeayo mikoani ya mjini Iringa, Samwel Yengayenga baada ya kuchomwa kisu mara mbili katika eneo la mgongoni na kifuani.
Tukio hilo la kinyama limetokea jana majira ya saa 6:.55 mchana baada ya Yengayenga na mtuhumiwa wa mauaji yake aliyekuwa akidai kiasi hicho cha fedha kurushiana maneno makali na kisha kupigana.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Festo Ruben Mkalala (26), muosha magari, mkazi wa mjini Iringa ambaye alikamatwa mara baada ya kufanya tukio hilo.
Mungi alisema Yengayenga, Mkalala na mtu mwingine wa tatu (hakumtaja jina) wanadaiwa siku nne zilizopita waliosha basi la Kimotco linalofanya safari zake kati ya Iringa na Arusha.
“Stahiki ya kazi hiyo ilikuwa Sh 15,000; hata hivyo hawakulipwa fedha hizo baada ya kumaliza kazi hiyo,” alisema.
Alisema siku iliyofuata Mkalala na kijana huyo mwingine waliyefanya naye kazi walikwenda kuchukua ujira wao na kugawana Sh 5,000 kila mmoja huku Mkalala akiahidi kutunza Sh 5,000 za Yengayenga mpaka watakapokutana.
Walipokuta, RPC alisema Mkalala alimpa Yengayenga Sh 3,000 badala ya Sh 5,000 na kuahidi kummalizia kiasi kilichobaki kesho yake.
Kitendo hicho kwa mujibu wa mashuhuda kinadaiwa kumchukiza Yengayenga aliyeamua kunyanganya simu ya Mkalala mpaka amaliziwe Sh2,000 zake zilizobaki.
Kamanda Mungi alisema Mkalala alichukizwa na uamuzi huo na kuanzisha ugomvi uliopeleka kifo cha Yengayenga.
“Uchunguzi wa awali unaonesha Mkalala aliamua kupigana na Yengayenga ili arudishiwe simu yake na alipozidiwa alikimbia kusikojulikana na kurudi akiwa na kisu mkononi,” alisema.
Ili kuipata simu yake, Kamanda Mungi alisema ushahidi wa awali unaonesha Mkalala alitumia kisu hicho kumchoma mgongoni na kifuani Yengayenga na kusababisha mauti yake.
Yengayenga alikufa papo hapo katika tukio ambalo mtuhumiwa huyo alikamatwa na kufikishwa kituo cha Polisi cha kati cha mjini Iringa.
Na Frank Leonard -Iringa
SHILINGI ELFU MBILI YAPELEKEA MAUTI
Reviewed by habari motto
on
9:29 AM
Rating: