Wage ambaye ni mbaya wa Jerry Muro, mtangazaji maarufu aliyemtuhumu kuomba rushwa na mahakama kumuona hakuwa na hatia, alisimamishwa kazi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda mwaka 2013 akiwa na maofisa wenzie ili kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma za kuisababishia serikali hasara ya shilingi 221, 220,280.
Uchunguzi uliofanywa na paparazii katika Halmashauri ya Bagamoyo hivi karibuni, umebaini kuwa kesi hiyo inaendeshwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Wilaya ya Bagamoyo.
Chanzo chetu kililieleza paparazi kuwa kesi hiyo ilikuwa ianze kusikilizwa mwezi uliopita lakini jalada bado lipo kwa DPP na haijafahamika lini litafikishwa mahakamani.
Mtangazaji maarufuJerry Muro.
“Hii kesi inatutesa sana kwa sababu inachelewa kuanza... tatizo ni kwa DPP hatujui kuna nini,” alisema afisa mmoja wa Takukuru wilayani Bagamoyo aliyeomba jina lake lisiandikwe.
Akizungumza na paparazi ofisa huyo alisema kesi hiyo bado ipo isipokuwa kuna marekebisho kidogo yalifanyika na jalada kupelekwa kwa DPP kwa hatua zaidi.
Hata hivyo, uchunguzi wetu umebaini kuwa mmoja wa viongozi waliosimamishwa na Wage kwa tuhuma hizo ambaye baadaye aliachiwa na kurudishwa kazini akiwa ni Afisa Mipango wa Bagamoyo, Aloyce Gabriel (59) alikutwa amefariki dunia nyumbani kwake.
Marehemu Gabriel alikutwa na jirani yake mmoja akiwa amefariki Machi 11 , 2014 saa 2.30 usiku katika nyumba ya Shirika la Nyumba la Taifa aliyokuwa akiishi huku mwili wake ukiwa umeharibika.
Uchunguzi umebaini pia kuwa afisa huyo alikuwa ni shahidi muhimu upande wa serikali kwani alikuwa anajua vitu vingi ndani ya halmashauri hiyo.