Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC) limezungumzia sakata la maaskofu wa kanisa hilo, Methodius Kilaini na Eusebius Nzigirwa kudaiwa kupewa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow na kusema kwa sasa hawawezi kuzungumzia suala hilo kutokana na kuwa linagusa watu binafsi.
Limesema kuwa suala hilo halihusu baraza na inaweza kufanyiwa kazi kwa taratibu za kanisa kwa kadri uchunguzi unavyoendelea kufanyika, lakini sasa ni mapema mno.
Msemaji wa Baraza hilo, Padri Anatoly Salawa alisema kwa sasa suala hilo wazungumzaji ni watu binafsi ambao wanahusika katika sakata hilo na siyo kama baraza.
Alisema orodha inawahusu watu wengi na kwamba wakati mwafaka ukifika kanisa litatoa kauli, lakini suala hilo ni binafsi na askofu yeyote ana haki ya kufungua akaunti binafsi kama ilivyo kwa mtu yeyote.
Alisema suala hapo linalohusu kanisa ni Benki ya Mkombozi, lakini hata hivyo benki haina mamlaka ya kumuuliza mteja alipopata fedha mpaka watilie shaka na kutoa taarifa Benki Kuu ili kuchunguza.
Padri Salawa alikana taarifa zilizozagaa katika mitandao ya kijamii kuwa Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Bukoba, Methodius Kilaini aliitwa jijini Dar es Salaam kutokana na tuhuma hizo.
“Taarifa hizo siyo za kweli, kwani Askofu Kilaini yupo hapa jijini Dar es Salaam kufungua kongamano la kiroho la Afrika Mashariki alilofungua jana (juzi) katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu na mpaka sasa bado yupo,” alisema.
Baraza la Maaskofu lazungumzia 'mgawo wa escrow' kwa Makasisi wake
Reviewed by habari motto
on
4:03 PM
Rating: