Mjadala wa “maadili” ni jambo linalohitajika. Sio mjadala wa kubishana kuhusu kilicho sahihi na kisicho sahihi. Ni mjadala wa kueleweshana na kukumbushana tulipotoka, tulipo na tunapokwenda. Dunia imebadilika. Mwingilio mkubwa wa tekinolojia na kile ambacho wengine wanaweza kukiita “maendeleo na utandawazi”,yameigeuza dunia juu chini.
Mengi yanahitaji mjadala na ufafanuzi. Yanahitaji sheria na kanuni tofauti. Kuna ya kubadilika. Kuna ya kuendeleza nk. Suala la “maadili” limepanuka. Uzibe kipi uache kipi. Vigezo gani utumie? Kwanini? Nani ana mamlaka ya kusema hili sio na lile ndio? Yapo mengi. Naandaa makala.
Baada ya kusema hayo, hivi karibuni msanii Ney Wa Mitego alitoa wimbo ambao aliupa jina ‘Pale Kati Patamu”. Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) limetangaza kuupiga marufuku wimbo huo. Sababu wamezitaja kama ifuatavyo; Nimenukuu taarifa yao neno kwa neno.
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeufungia rasmi wimbo wa ‘pale kati patamu’ ulioimbwa na Msanii Ney wa Mitengo kutokana na ukiukwaji mkubwa wa maadili.
Msanii huyu amekuwa na tabia na mienendo yenye kuchafua Sekta ya Sanaa yeye binafsi kupitia kutoa kazi chafu na kufanya maonesho yenye kukiuka maadili. Kazi zake zikikiuka maadili na kudhalilisha utu wa mwanamke sambamba na kutoa lugha za matusi na za kudhalilisha watu wa kada mbalimbali.
Ieleweke kwamba kwa mujibu wa kifungu namba 4(L) cha Sheria ya BASATA namba 23 ya mwaka 1984, Baraza limepewa jukumu la kuhakikisha linalinda maadili miongoni mwa wasanii wanapokuwa jukwaani au wanapobuni kazi yoyote ya sanaa.
Ikumbukwe kwamba BASATA limeshamuita na kumuonya msanii huyu mara kadhaa kutokana na tabia yake ya kutoa kazi zisizokuwa na maadili na aliahidi kubadilika na kuachana na tabia hiyo. Kwa hiyo kuendelea kwake kufanya matukio haya kwa makusudi ni uthibitisho kwamba hajabadilika na kwa maana hiyo ameendelea kuidhalilisha Sanaa na wasanii wa kitanzania wenye kujitambua na kuiheshimu kazi ya sanaa kama kazi nyingine. Kwa sasa Msanii huyu ametoa wimbo mwingine wa Pale Kati patamu ambao uko mitandaoni ukipambwa na picha chafu zinazoonesha mwanamke akiwa mtupu yaani uchi wa mnyama.
Kwa mantiki hii BASATA halitavumilia wasanii wachache ambao wanataka kuigeuza tasnia ya sanaa na wasanii genge la wahuni wasio na staha na wanaojipanga kuibomoa jamii. BASATA linapenda kueleza ya kufuatayo
Aidha, BASATA linawataka Wasanii wote nchini kufuata sheria, kanuni na taratibu mara wanapotengeneza kazi zao.
- BASATA linatamka kuwa limeufungia wimbo huu rasmi kutumika kwa namna yoyote ile.
- Aidha pamoja na adhabu ya kufungia wimbo huu hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
SANAA NI KAZI, TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI.
Ney Wa Mitego Matatani Na Baraza La Sanaa Tanzania (BASATA)
Reviewed by habari motto
on
7:35 AM
Rating: