
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda (kulia) Bi. Janeth Mayanja akiangalia moja ya kihenge kilichokua kimehifadhi mazao ambayo yameshambuliwa na tembo katika kijiji cha Tamau kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Bunda, mkoani Mara.
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Wilaya ya Bunda, mkoani Mara iko katika hatari ya kukumbwa njaa kufuatia tembo kuvamia vijiji mbalimbali na kula mazao yaliyopo mashambani pamoja na yaliyohifadhiwa katika vihenge.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, mkoani Mara, Bi. Janeth Mayanja alisema kuwa tembo wamekuwa wakivamia mashamba na kula mazao yaliyohifadhiwa kwenye vihenge katika vijiji vya Kunzungu, Nyatwali, Tamau, Serengeti, Kinyambwiga, Balili na Mihale kiasi ambacho kinaweza kusababisha njaa katika katika vijiji hivyo.
“Kwa takwimu za mwezi huu tu zaidi ya wakulima 30 mashamba yao yamevamiwa na mazao yao yameliwa na tembo, hivyo ninaiomba Wizara ya Maliasili na Utalii ichukue hatua za haraka kukabiliana na changamoto hii” alisema Bi. Mayanja.
Ameongeza kuwa, mwaka 2012 tembo walivamia vijiji jirani ndani ya Wilaya ya Bunda kwa upande wa kusini wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambapo waliharibu mazao kadhaa yaliyokuwemo mashambani na kwenye vihenge, hata hivyo taarifa zilipelekwa katika wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kufanya tathimini ili kuwalipa fidia wakulima walioharibiwa mazao yao, hata hivyo fidia haikupatikana kwa wakati kitu ambacho kilisababisha tatizo la njaa katika maeneo hayo.
Bi. Mayanja ameiomba wizara husika ifanye utafiti wa kina kujua ni kwa nini miaka ya hivi karibuni tembo wamekuwa wakivamia kwa wingi katika vijiji vya wilayani Bunda ikiwa ni katika kupatia ufumbuzi tatizo hilo.Mazao yaliyoliwa na tembo katika vijiji hivyo ni pamoja na mihogo, mahindi, mtama na mpunga.
Bunda Hatarini Kukubwa Na Janga La Njaa
Reviewed by habari motto
on
1:01 PM
Rating:
