Azam FC Imetamka kuwa haipo tayari kumuachia beki wao wa kati, Said Morad kujiunga na Simba inayomhitaji katika usajili wa dirisha dogo katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara. Kauli hiyo imetolewa ikiwa ni siku chache baada ya kuwepo na tetesi za Simba kuomba kubadilishana na beki huyo na kiungo mshambuliaji mkongwe wa Msimbazi, Amri Kiemba aliyesimamishwa na uongozi wa timu hiyo. Awali, Azam FC ndiyo iliyoanza kumuomba Kiemba kwa mkopo baada ya uongozi wa Simba kumfungia pamoja na wenzake, Shaaban Kisiga na Haroun Chanongo kwa kile kilichodaiwa utovu wa nidhamu waliouonyesha wakiwa Mbeya wakijiandaa na mechi dhidi ya Tanzania Prisons. Akizungumza na Championi Jumamosi, Mwenyekiti wa Azam FC, Said Mohamed, alisema hawatakubali kumuachia beki huyo kutokana na kumhitaji, licha ya kumsajili beki mwingine Muivory Coast, Serge Wawa aliyetokea El-Mereikh ya Sudan. Said alisema, wao wamemuomba Kiemba pekee katika usajili wao baada ya kupokea mapendekezo ya kocha wao Mcameroon, Joseph Omog kutokana na aina ya kiungo anayemhitaji katika kukiimarisha kikosi chake na siyo kubadilishana. Aliongeza kuwa, Simba kama hawataki kumtoa kwa mkopo Kiemba basi, lakini siyo kubadilishana, hivyo beki atabaki kuendelea kuichezea timu hiyo katika raundi ya nane ya ligi kuu iliyosimama. “Sisi tulimuomba Kiemba kwa mkopo na siyo kumnunua kwa jumla na beki wetu Morad haendi popote, atabaki kuendelea kuichezea Azam FC kutokana na kuwepo kwenye mipango na kocha wetu Omog,” alisema Said. Imeelezwa pamoja na kuwa na mabeki wengi wa kati, Azam FC imeonekana haina uhakika kama Serge Wawa iliyemsajili kutoka Sudan atazoea haraka mazongira ya Tanzania. Hivyo itaendelea kubaki na Morad, halafu itaangalia kama inaweza kumuachia mwishoni mwa msimu. Source;Championi
Azam kutomuuza Morad
Reviewed by habari motto
on
1:44 PM
Rating: