Pinda kuwa muungwana jasiri ujiuzulu

SITII chumvi. Lakini ukweli ni kwamba lau serikali ya sasa ya Tanzania ingelikuwa inajiheshimu basi siku hii ya leo serikali hiyo ingekuwa inaongozwa na Waziri Mkuu mwengine asiye Mizengo Pinda.
Pinda, anayejigamba kwamba ni mtoto wa mkulima,aliwajibika kujiuzulu Novemba 17 mara tu baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Public Accounts Committee) kukabidhiwa na Naibu Spika, Job Ndugai, vitabu vitano vya ripoti ya uchunguzi wa tuhuma za kashfa ya IPTL.
Kamati hiyo huteuliwa na Bunge na imepewa dhamana ya kuzikagua hesabu za serikali na jinsi serikali inavyozitumia fedha hizo ambazo kwa kweli ni fedha za umma, za kila Mtanzania. Kwa sasa kamati hiyo iko chini ya uenyekiti wa Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Kisa na mkasa wa kashfa hiyo ni shilingi 306 bilioni zilizochotwa kutoka akaunti ya escrow iliyo Benki Kuu ya Tanzania. Akaunti za aina ya escrow huwa na rubuni au fedha zilizowekwa kama amana katika taasisi ya tatu (mfano Benki Kuu) kwa niaba ya pande mbili zilizoandikiana mkataba wa kibiashara.
Fedha hizo zilizochotwa zilikuwa zimewekwa amana katika Benki Kuu ya Tanzania zikiwa gharama za uwekezaji kwa Shirika la Kufua Umeme la IPTL. Zilifunguliwa akaunti hiyo baada ya IPTL kuzozana na Tanesco (Shirika la Umeme la Tanzania).
Mzozo wenyewe ulianza pale Tanesco ilipolalamika kwamba imekuwa ikiilipa IPTL fedha zaidi ya gharama zake za uwekezaji. Ndipo Mahakama ilipoamua kwamba fedha ambazo Tanesco ilitakiwa ilipe ziwekwe kwenye akaunti ya escrow.
Februari 12 katika hukumu yake Mahakama ilikubali kwamba kweli Tanesco ilikuwa ikililipa shirika la IPTL fedha zaidi. Na ilibainika kwamba fedha zilizokuwa zimewekwa amana katika akaunti ya escrow zilikuwa zimechotwa, kinyume na sheria. Kwa hakika, uchotaji huo ni wizi mtupu.
Hali kadhalika, ilidhihirika kwamba waliozichota au waliozidokoa fedha hizo walipewa ruhusa ya kufanya hivyo na baadhi ya viongozi wa juu wa serikali ya Tanzania. Hivi ni kusema kwamba ni viongozi wa serikali walioshiriki katika wizi huo.
Mwenye dhima ya uongozaji wa shughuli za kila siku za serikali ni Waziri Mkuu. Katika mfumo wa utawala tulionao Waziri Mkuu ndiye mwenye kuwajibika kwa matendo ya serikali — yawe ya mawaziri au ya viongozi wengine wakuu serikalini. Bila ya shaka yeye ndiye mwenye kuwajibika kwa matendo yake mwenyewe.
Kwa kawaida, pakitokea kashfa kama hii ya kuchotwa fedha kutoka akaunti ya escrow kashfa hiyo kuzusha mgogoro wa kisiasa. Kiongozi wa serikali huwa hana hila ila kumuandika Rais wa nchi barua nzuri ya heshima na kwa unyenyekevu akajiuzulu.
Hufanya hivyo hata ikiwa yeye mwenyewe binafsi hakuhusika na kashfa hiyo seuze akiwa amehusika. Hiyo ndiyo maana ya “kuwajibika.” Kiongozi huchukuwa dhamana ya uzembe uliopelekea pakazuka kashfa kama hiyo.
Mheshimiwa Pinda, akiwa mwanasheria na mwanasiasa aliyepevuka, anayajuwa hayo vizuri. Lakini bado amezing’ang’ania hatamu za serikali. Hataki kuziachia.
Katika mfumo wa utawala wenye kujiheshimu lau kama Waziri Mkuu anadinda na anakataa kujiuzulu basi Mkuu wa Taifa, na kwa Tanzania ni Rais, hufanya maarifa ya kumshawishi Waziri Mkuu awe mnyenyekevu na ajiuzulu. Mpaka sasa tujuavyo Rais hakufanya hivyo.
Kuna tafsiri moja ya yote hayo ya Waziri Mkuu na Rais wake. Nayo ni kwamba inavyoonyesha wote wawili wanawadharau wananchi. Hawawajali.
Tutasikia siku chache zijazo kwamba wakuu wawili watatu wa serikali wamefukuzwa kazi kwa kuhusika na kashfa hiyo ya akaunti ya escrow. Watakuwa ni vijidagaa tu katika bahari ya ufisadi. Ile mipapa inayotamba na kuelea katika bahari hiyo itaendelea na shughuli zao kana kwamba hakuna la karaha lililotokea.
Tanzania itapiga hatua mbele ikiwa haya niliyoyaandika hayatokuwa sahihi na tukiishuhudia mipapa ya ufisadi ikichukuliwa hatua zifaazo na wale wanaowajibika, akiwemo Waziri Mkuu, wakijiuzulu.
Ingawa hatuyatarajii lakini hayo yanaweza kutokea kwani Tanzania imetoka mbali tangu ilipokuwa taifa lenye mfumo wa chama kimoja cha siasa na Bunge lenye kukiwakilisha chama hicho kimoja tu.
Kuna wakati Bunge hilo likiviwakilisha vyama viwili — Tanganyika African Union(TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP), pale TANU kilipokuwa chama pekee kilichokuwa halali Tanzania Bara na ASP kilipokuwa chama pekee Zanzibar.
Hayo yalikuwa katika zama ambapo Tanzania chini ya Mwalimu Julius Nyerere ikifuata siasa za Nyerere za Ujamaa na Kujitegemea.
Ingawa utawala wa Nyerere ulikuwa na madosari yake hata hivyo utawala huo haukuwahi hata mara moja kunuka ufisadi kama hali ilivyo hivi sasa. Unaweza ukamsema Nyerere kwa mengi lakini si kwa hili.
Alizitunga sera zake akiamini kwa dhati kwamba zitamkomboa mwananchi wa kawaida. Hata ile sera yake ya kuwa na utawala wa chama kimoja tu cha siasa akiiamini kwa dhati kuwa inaweza kuwa na utawala wa kidemokrasia. Ndipo alipounda Tume maalum kuzingatia Kuundwa kwa Taifa La Kidemokrasia La Chama Kimoja.
Wakati huo Bunge lilikuwa likizorota, mijadala yake ilikuwa chapwa ikijadili mambo kijuu juu tu si kwa kina, sheria zikitungwa na wabunge wakizipitisha haraka haraka bila ya kuzizingatia kwa makini. Kanuni za msingi za Bunge pia zilikuwa hazifuatwi.
Katika hali hiyo kulikuwa na hatari kwamba Bunge ama lingeozeana au lingekufa. Mwalimu Nyerere akahoji kwamba pengine ni bora kulitoa Bunge kutoka kwenye mfumo wa utawala wa dola na badala yake liingizwe kwenye makucha ya chama kinachotawala.
Baada ya kufanya uchunguzi wake Tume aliyoiunda iligundua kwamba Bunge halikuwa mahututi lakini lilizubaa kwa vile lilikosa mashindano na mabishano baina ya vyama vya siasa. Juu ya yote hayo lilikuwa na dhima ya wazi na muhimu katika mfumo wa chama kimoja cha siasa.
Tume iliamini kwamba ikiwa chama cha TANU kitatambuliwa kisheria kuwa ndicho chama pekee kilicho halali kutalifanya Bunge lichipuke upya na kuendelea na shughuli zake za kibunge.
Tume hiyo ilikuwa na dhamiri za dhati za kulifanya Bunge liwe mahali muhimu ambapo wananchi watazionyesha nguvu zao kupitia wawakilishi wao, yaani wabunge. Tume ilionyesha dhamiri zake kwa mapendekezo iliyoyatoa kuhusu namna ya kuufanya uwe bora zaidi utendaji kazi wa Bunge.
Moja ya mapendekezo hayo ni lile la kuundwa kwa kamati maalum za utungaji sheria.
Kwa hivyo, hatua ya kuifanya nchi iwe taifa lenye chama kimoja tu cha siasa ilikuwa ni hatua ya kuuendeleza mkakati wa TANU wa tangu siku za kuwania uhuru. Mkakati huo ulihusika na namna ya kukifanya chama hicho kishinde katika uchaguzi wa “mtu mmoja kura moja”, ushindi ambao utakifanya chama hicho kilidhibiti Bunge.
Huo udhibiti wa Bunge ukionekana kuwa ndio mlango wa kuingilia utawala wa kisiasa. Mwenye kulidhibiti Bunge ndiye mwenye nguvu, mwenye mamlaka na madaraka ya kutawala. Ilikuwa ni sawa na haki kufanya uchaguzi wa Bunge kwa sababu lengo la uchaguzi ni kumuwezesha mshindi awe na nguvu za kisiasa.
Hayo yalikuwa ya Bunge katika enzi za mfumo wa chama kimoja. Katika kipindi kizima cha mfumo huo wa utawala wa chama kimoja Bunge likijaribu kuendesha shughuli zake kwa kuwatetea wanyonge.
Bunge lilijaribu lakini halikufanikiwa kama hivi sasa ambapo wabunge wa chama kinachotawala na wa upinzani wanaposhikamana, kwa mfano, kuupinga ufisadi.
La ajabu, na la kusikitisha, ni kwamba juu ya kuwa kumetokea visa kadhaa vya kashfa za viongozi wa serikali nchini Tanzania katika miaka hivi karibuni hatukushuhudia bado kiongozi ye yote wa ngazi ya juu aliyefikishwa mahakamani na kupewa adhabu anayostahiki kupewa. Watu wamefukuzwa makazini na wameachiwa wende wakastarehe na fedha walizoziiba.
Rais naye amekuwa akiteua mawaziri na wasaidizi wake wengine wakuu wenye ukosefu wa uadilifu. Baadaye baadhi yao hawakuweza nao kujizuia ila waliuvaa ufisadi.
Tuliyemdhania siye kumbe ndiye. Tunayemdhania hayumo kumbe yumo na amejaa tele katika dimbwi la ufisadi. Wengine ni waheshimiwa waliowahi kusifika kwa kuongoza mashirika ya kimataifa.
Kwa kawaida, lila na fila havitengamani lakini sio katika serikali ya Tanzania. Humo vyote ni sawa. Idadi ya kashfa zilizowameza viongozi wa serikali si ndogo.
Wananchi wanapiga kelele lakini viongozi wakuu wa serikali hawawasikilizi. Wamo mbioni kutoa udhuru wa kuhalalisha madhambi yao. Au kama hawafanyi hivyo basi wanakuwa mbioni kuandaa njama za kuyaficha madhambi hayo na kuubabaisha umma.
Inafaa Pinda alipe heshima taifa na aonyeshe uungwana na ujasiri wa kujiuzulu. Kama hataki basi Rais amfungulie mlango na amwonyeshe pa kwenda.
Wakifanya hivyo watakuwa wanaliheshimu taifa na wanajiheshimu wenyewe. Ubaya wa mambo ni kwamba waheshimiwa wa serikali hii hawajiheshimu.
Tena hawana haya wala hawajui vibaya.
Chanzo: Raia mwema
Pinda kuwa muungwana jasiri ujiuzulu Pinda kuwa muungwana jasiri ujiuzulu Reviewed by habari motto on 9:59 AM Rating: 5
ads 728x90 B
Powered by Blogger.