UMESIKIA KUHUSU NJAMA ZA KUMUUA SILAA: NI ZAIDI YA MASELE


      12  
 Taarifa za kuchukiza na kutisha kuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) 
mbunge wa Shinyanga Mjini na Waziri mdogo (Nishati na Madini) Steven Masele 
pamoja na wenzake, walipanga na kuratibu mpango mchafu wa kuwaua Katibu
 mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Wilbroad Slaa
 na Mkurungenzi wa Mawasiliano na Uhusiano, mbunge wa Ubungo, John Mnyika zinaiweka CCM pabaya. Je Masele ni nani? Je yuko peke yake katika ugaidi huu 
unaoonekana kupangwa na watu wengi zaidi yake? Je atachukuliwa hatua au 
kufumbiwa macho kama mwenzake, Mbunge wa Iramba na Waziri mdogo wa Fedha, Mwigulu Nchemba, aliyetuhumiwa kwa vitendo vya kigaidi akapandishwa cheo? 
Je imeishia wapi kesi ya kubambikizwa ya mkurugenzi wa usalama wa CHADEMA,
 Wilfred Rwakatare? Si wameuia kimya kimya baada ya mbinu zao za kigaidi 
kufichuliwa? Je watanzania wataendelea kujiruhusu kutawaliwa na chama
 kilichoishiwa kiasi cha kujigeuza kundi la kigaidi? Je njama kama hii ingeelekezwa 
kwa Katibu mkuu wa CCM Abdulrahaman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, 
Nape Nnauye serikali ingeendelea kujifanya hamnazo wala haijui kitu? Mbona
 tunatumia sheria kihuni na kibaguzi hivi?
          Diwani wa kata ya Ngokolo mjini Shinyanga, Sebastian Peter alifichua kuwa
 waliahidiwa mamilioni ya fedha kutekeleza mauaji ya wawili tajwa walipokuwa 
Shinyanga kikazi mwezi Februari. Peter alikaririwa akisema, “Baada ya maongezi 
ya aina mbali mbali na Mchange tulishindwa kupata muafaka lakini tuliendelea 
kuwasiliana na aliporudi Shinyanga akatueleza kuwa kuna mpango mzuri wa fedha 
na kwamba utasimamiwa na Waziri Masele na kwamba tutapata sh. milioni 180 
kila mmoja.” Hivi kweli kuna ushahidi zaidi ya huu kupaswa kumfungulia mashtaka
 Masele na wenzake? Kama huu ni uzushi mbona mtuhumiwa haendi mahakamani kusafisha jina lake? Peter anaendelea, “Mkakati huo ulianza kuratibiwa na Mwenyekiti wa 
UVCCM, Abbakari Gulam ambaye ni mtoto wa Meya wa Shinyanga, wakiwa na 
Habib Mchange, kisha tuliona mkakati unatekelezwa na mbunge wa Shinyanga 
mjini, Stephen Masele, Nape Nauye, Januari Makamba, Mwigulu Nchemba na 
Ridhiwani Kikwete.”
          Kwanza, ni aibu kwa mbunge, anayepaswa kuwa mfano wa jamii, kugeuka 
gaidi. Pia ni aibu kwa serikali kutochukua hatua stahiki. Kitendo cha Masele 
kushiriki ugaidi na uvunjaji wa sheria licha ya kumuaibisha kama mwakilishi wa 
wananchi, kinawaibisha na kuwadhalilisha wale waliomwamini uwakilishi. Pia,
 kwa nafasi yake, Masele alipaswa abanwe aachie ngazi kwa vile ameaibisha kazi ya
 ubunge na bunge kwa ujumla.  Mbunge anayeweza kupanga kutekeleza ugaidi 
hapaswi kuendelea kuwa bungeni wala uraiani bali gerezani akingojea kesi yake
 kusikilizwa na kutolewa hukumu. Kunajengeka dhana kuwa Masele alitumwa na
 wenye serikali inayomilki taasisi na vyombo vyote, hatachukuliwa hatua. Ndiyo 
maana mamlaka hazimchukulii hatua. Je kweli Tanzania inafaa kuendelea
 kutawaliwa na chama na serikali na watu wanaoweza kudiriki kutenda ugaidi 
halafu wakaendelea kulindana?
          Pili, kwa wanaojua uhusiano  baina ya Masele na mtoto wa kigogo mkubwa
 wa CCM ambaye pia ni kigogo wa serikali, hawashangazwi na hisia kuwa 
anatumiwa tu na mtandao mkubwa. Wengi wanajua kuwa, pamoja na udhaifu 
wake kitaaluma, Masele aliteuliwa kwenye nafasi aliyo nayo kutokana na ukaribu 
wake na mtoto wa kigogo huyu ambaye ana ushawishi mkubwa katika masuala
 mengi yanayohusiana na mamlaka ya baba yake. Pia kwa wanaojua makundi ya 
kigaidi yanavyofanya kazi, Masele hawezi kuwa peke yake. Lazima kuna watu 
wakubwa na makundi makubwa yaliyomtuma kupanga njama hizi. Huenda ndiyo
 maana akapigiwa kampeni na kuteuliwa uwaziri wakati hana sifa. Walimuopoa 
mapema wakijua wanavyoweza kumtumia wakati ukitimu.
          Tatu, siasa za kichovu, kikatili na kuishiwa sera tulizoea kuzisikia na
 kuzishuhudia kwa majirani zetu hasa Kenya ambapo chama tawala cha wakati ule 
kiliwaua makada wake wengi kiliodhania walikuwa tishio kwa ulaji wa bwana
 mkubwa. Pia, tulizoea kusikia watoto wa watawala wa huko nao wakijigeuza 
watawala tusijue yatafika hata kwetu. Je imekuwaje tumefika hapa? Bila shaka,  
ni matokeo ya ufisadi na siasa za kifisi ambapo kila mwenye kupata madaraka
 huyatumia vibaya kuibia umma na kujitajirisha kiasi cha wasaka tonge kuwa tayari
 kuua watu wasio na hatia ilmradi wapate madaraka ambayo ni hati ya kuibia umma
 kwao. Hivyo, si ajabu kushuhudia magaidi, majambazi hata wauza mihadarati 
wakijitokeza kutumia fedha zao zitokanazo na jinai yao kusaka nafasi za kisiasa na kuendeleza jinai yao bila kuguswa wala kuzuiliwa hata kama ni kwa kuua wenzao.
          Nne, wahanga wa mpango huu mchafu na CHADEMA wanapaswa kuomba 
vyombo vya kimataifa vinavyoshughulikia ugaidi kuingilia kati kwa sababu
 mamlaka za Tanzania haziwezi kufanya hivyo kutokana na kutekwa na CCM.
          Tano, watanzania wajulishwe kupitia mikutano mbali mbali aina ya utawala 
unaoanza kujengeka chini ya CCM ambayo imeamua, kwa tamaa ya madaraka,
 kujigeuza kuwa kundi la kigaidi. Chama kilichofikia kiwango hiki hakipaswi
 kuendelea kuvumiliwa kuwa madarakani. Kuna haja ya kuwahakikisha taasisi za 
kimataifa zinazoshughulikia ugaidi zinajulishwa angalau zitoe maelekezo hata 
maoni yake.
          Sita, walengwa wasijue yamekwisha. Wanapaswa kuchukua hatua madhubuti
 na tahadhari vya hali ya juu kwa vile kilichowasukuma CCM kutaka kuwaua bado 
kipo pale hasa ikizingatiwa kuwa CHADEMA ndiyo tishio lao. CCM iko tayari 
kufanya lolote liwe haramu au halali kuhakikisha inabakia madarakani ikifanya
 ufisadi na ugaidi wake kama kawaida. Hili halivumiliki. Upinzani unapaswa 
kulichukulia tishio hili kwa uzito unaostahili.
          Saba, kwa upande wake, licha ya kushinikiza Masele na genge lake la kigaidi
 lishitakiwe, kuna haja ya kumbana rais kuhakikisha anamwajibisha ili iwe rahisi kumshughulikia kisheria.
          Tumalizie kwa kulaani mchezo huu mchafu ambao kama hautazuiliwa kwa 
nguvu ya umma unaweza kulitumbikiza taifa kwenye machafuko na mauaji ambayo yangeweza kuzuilika.  Wakati wa kuzuia zahama hii ni sasa.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 27, 2014.

UMESIKIA KUHUSU NJAMA ZA KUMUUA SILAA: NI ZAIDI YA MASELE UMESIKIA KUHUSU NJAMA ZA KUMUUA SILAA: NI ZAIDI YA MASELE Reviewed by habari motto on 3:37 PM Rating: 5
ads 728x90 B
Powered by Blogger.