Hizi Ni Hatua 5 Muhimu Za Kutengeneza Wazo Bora La Biashara


Good-business-ideas Kutokana na hali ngumu ya kiuchumi na ukosefu wa ajira, kujiajiri imekuwa njia bora ya kujipatia kipato. Watu wengi wanasukumwa kuingia kwenye biashara au ujasiriamali kutokana na kukosa ajira au kipato cha ajira kuwa kidogo ukilinganisha na gharama za maisha.  Ili kuweza kufanikiwa kwenye biashara unahitaji kuwa na wazo zuri la biashara. Je unajua jinsi ya kupata wazo hilo zuri la biashara? Watu wengi wamekuwa wakiomba ushauri ni wazo gani zuri la biashara ambalo linaweza kuwapatia faida na mafanikio. Ukweli ni kwamba wazo ambalo ni bora kwa mtu fulani linaweza lisiwe bora kwako. Moja ya sababu zinazofanya biashara nyingi kufa au kutokuendelea ni kuiga, yaani mtu akianza biashara leo baada ya muda unakuta watu wengine wameiga biashara ile ile, wanaifanya eneo lile lile na kwa mbinu zile zile. Hii ni njia rahisi sana ya kushindwa kwenye biashara. Leo tutajadili njia tano unazoweza kutumia kupata wazo bora la biashara ambayo itakupatia mafanikio makubwa. Kwa kutumia njia hizi utatengeneza wazo lako mwenyewe na utaweza kulifanyia kazi vizuri sana. Zifuatazo ni njia tano unazoweza kupitia katika kutengeneza wazo zuri la biashara: 1. Unapenda vitu gani? Kila mmoja wetu kuna vitu ambavyo anavipenda sana. Vitu hivi vinaweza kuwa ni vipaji vyako au ni vitu ambavyo umetokea kuvutiwa navyo na hivyo kupenda kuvifuatilia. Inawezekana unapenda mitindo, unapenda kutumia intaneti, unapenda kujifunza zaidi, unapenda watoto, unapenda magari au unapenda michezo fulani. Orodhesha vitu vyote ambavyo unapenda kuvifanya na unapenda kuvifuatilia. Hakikisha vitu unavyoorodhesha unavipenda kweli na upo tayari kuvifanya hata kama hulipwi fedha. 2. Una ujuzi au uzoefu  gani? Katika maisha yako kuna ujuzi au uzoefu ambao umeupata. Yawezekana umesomea fani fulani au umewahi kufanya kazi ambayo ilikupatia ujuzi fulani. Orodhesha ujuzi wote ambao umeupata kutoka kwenye elimu na hata kujisomea au kufuatailia watu waliofanikiwa. Pia orodhesha uzoefu wowote ambao umewahi kuupata kwa kazi ambazo umewahi kufanya, iwe ni ajira kujiajiri au hata kujitolea. 3. Watu wanaokuzunguka wana matatizo gani? Angalia jamii inayokuzunguka ina matatizo au changamoto gani ambazo watu wako tayari kulipa kama kutakuwa na suluhisho. Angalia changamoto ambazo zinaendana na vitu unavyopenda kufanya  na ujuzi au uzoefu wako. Ni rahisi sana kuzijua changamoto za jamii inayokuzunguka kama unaishi kwenye enao hilo na itakuwa rahisi zaidi kwako kuwashawishi kufanya biashara na wewe. Kila jamii ina changamoto zake hivyo kama ukifikiri na kuchunguza vizuri utapata changamoto nyingi za jamii inayokuzunguka. 4. Angalia biashara nyingine zinazokuzunguka. Baadha ya kujua changamoto zinazowakabili watu kwenye jamii yako angalia biashara ambazo zinafanyika kwenye eneo hilo ambazo zinajaribu kutatua changamoto hizo. Jifunze biashara hizo kwa undani sana, jua uimara wao uko wapi na mapungufu yao yako wapi. Jua ni vitu gani ambavyo wanakosa  na wewe unaweza kuvitoa kwa ubora wa juu sana. Pia jua ni malalamiko gani ambayo wateja wanatoa kwenye biashara hizo au ni vitu gani wateja wanataka lakini wanakosa. 5. Kamilisha wazo lako la biashara lenye ubunifu mkubwa. Baada ya kuorodhesha vitu ambavyo unapenda kuvifanya na kuorodhesha ujuzi au uzoefu uliowahi kuupata, changanya vitu hivi viwili na uone ni jinsi gani watu wanaweza kukulipa kwa kitu kimoja unachopenda kufanya na una ujuzi au uzoefu fulani. Baada ya kuamua kitu kimoja ambacho utakifanya na kujiridhisha kwamba watu wanaweza kukulipa kwa kufanya kitu hiko angalia matatizo au changamoto ambazo zinawakabili watu wanaokuzunguka. Angalia jinsi ambavyo kitu ulichoamua kufanya kinaweza kutatua matatizo au changamoto hizo. Angalia wanaofanya biashara kama hiyo ambayo unayotaka kufanya wana ubora gani na mapungufu gani. Baada ya yote haya sasa unaweza kukamilisha wazo lako la biashara kwa kuweka vitu tofauti na wale wanaofanya biashara hiyo. Kuwa mbunifu na weka utofauti ili uweze kupata wateja wengi zaidi na kufanikiwa kupitia biashara hiyo. Kwa kutumia njia hizo tano hapo juu unaweza kupata wazo bora kabisa la biashara. Kumbuka wazo bora la biashara ni sehemu ndogo sana ya mafanikio ya biashara, sehemu kubwa ya mafanikio ya biashara inatokana na kufanya kazi kwa bidii na maarifa na pia kuwa na uvumilivu mkubwa. Uzuri wa kutengeneza wazo lako la biashara ni kwamba itakuwezesha kuwa na uvumilivu pale mambo yatakapokuwa magumu kwa sababu unachofanya ni kitu ambacho unakipenda. Nakutakia mafanikio makubwa kwenye biashara yako
Hizi Ni Hatua 5 Muhimu Za Kutengeneza Wazo Bora La Biashara Hizi Ni Hatua 5 Muhimu Za Kutengeneza Wazo Bora La Biashara Reviewed by habari motto on 8:03 PM Rating: 5
ads 728x90 B
Powered by Blogger.