Ajiua Kisa Kulazimishwa Ndoa, Aacha Ujumbe Masikioni

Mkazi wa Kijiji cha Duga Horohoro mkoani Tanga, Mbito Dilima amejiua kwa kujinyonga akitumia chandarua na kuacha ujumbe kuwa, sababu ya uamuzi huo ni kulazimishwa kuoa mwanamke asiye chaguo lake.

Kaimu kamanda wa polisi wa mkoani Tanga, Juma Ndaki alisema mtu huyo alijinyonga akiwa chumbani kwake juzi saa 2:00 usiku.
Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa, marehemu alichukua uamuzi wa kusitisha uhai wake kutokana na wazazi wake kumlazimisha kwa muda mrefu kumuoa binti ambaye hakumpenda, hivyo kuibua mzozo wa kifamilia.
Ndaki alisema karatasi iliyoandikwa ujumbe huo aliiweka sikioni kama msokoto wa sigara na kwamba wanaendelea na uchunguzi zaidi ili kujiridhisha na ukweli wa ujumbe aliouacha marehemu.
“Uchunguzi wetu, kwanza ni kuwahoji wazazi wa marehemu na kupata ushahidi mwingine kutoka kwa majirani kama utakuwapo,” alisema Ndaki.
Katika tukio jingine, Ndaki alisema kuwa dereva wa bodaboda, Juma Said alinusurika kuuawa na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi.
Watu hao walimkodi kijana huyo kabla ya kumvamia na kumpiga kwa lengo la kupora chombo chake cha moto, jaribio ambalo lilishindikana.
Kamanda Ndaki alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 6:00 usiku katika maeneo ya Magomeni, mjini Tanga.
Alisema wakati wakibishana na kutishia kupigana, mmoja wa majambazi hao alitoa sime na kumtaka aondoke ili aepuke kukatwa mikono na miguu yote.
Alitoa wito kwa madereva hao wa bodaboda kuwa na umoja na kufanya mawasiliano katika vituo vyao, hasa anapotokea mmoja wao kukodiwa nje ya mji wakati wa usiku.
Ajiua Kisa Kulazimishwa Ndoa, Aacha Ujumbe Masikioni Ajiua Kisa Kulazimishwa Ndoa, Aacha Ujumbe Masikioni Reviewed by habari motto on 4:56 PM Rating: 5
ads 728x90 B
Powered by Blogger.