Wakati maazimio nane yaliyotolewa na Bunge kwenye mkutano wa 16 na 17 mwishoni mwa mwaka jana kuhusiana na kashfa ya uchotwaji fedha zaidi ya Sh. Bilioni 300 za akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yakiwa hayajatekelezwa yote, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, amesema watu waliofikishwa mahakamani katika sakata hilo ni dagaa tu na kwamba kambare (vigogo) wanaendelea kutanua.
Aidha, wabunge wengine wawili kutoka miongoni mwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamesema Mkutano wa 18 wa Bunge ujao watawasha moto kama Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo hatakuwa amewajibishwa ama kujiuzulu mwenyewe.
Kafulila alisema hayo juzi wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi wa kata ya Tubuyu, Manispaa ya Morogoro ulioitishwa Ukawa kwa ajili ya kuwapongeza viongozi mbalimbali walioshinda uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Alisema watuhumiwa watano walioanza kufikishwa mahakamani wiki iliyopita ni sawa na dagaa huku kambare wakiendelea kulindwa kwa maslahi ya baadhi ya viongozi wa Serikali.
Alisema vigogo wakuu wa sataka hilo ni pamoja na Profesa Muhongo; Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Alisema inashangaza kuona hadi sasa vigogo hao hawajachukuliwa hatua ikiwamo ya kufukuzwa kazi, kurudisha fedha hizo pamoja na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Kafulila alitolea mfano aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba, kuwa wakati wa uongozi wake alisamehe kodi ya Sh. bilioni 11.7, lakini alifikishwa mahakamani kutokana na tuhuma hizo na mpaka sasa kesi hiyo inaendelea.
“Kwanini watuhumiwa wa sakata la Tegeta Escrow ambao ni vigogo wanaofahamika hawachukuliwi hatua, badala yake wanafikishwa mahakamani watu wa ngazi ya chini?” alihoji.
Aliongeza kuwa kutokana na sakata hilo, Tanzania imekosa fedha za misaada ya miradi ya maendeleo zaidi ya Sh. bilioni 900 kutoka nchi za Ulaya na Sh. bilioni 1,200 za miradi ya Milenium Challenge (MCC) kutoka Marekani.
Alisema hali hiyo imepelekea hivi sasa Watanzania kukosa huduma muhimu ikiwamo ya dawa katika hospitali nchini na hivyo kupelekea baadhi yao kufa baada ya kukosa huduma hizo.
Kafulila alisema katika Mkutano ujao wa 18 wa Bunge Januari 27, mwaka huu, ameshawasilisha kusudio katika ofisi ya Spika wa Bunge la kuomba Ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ifikishwe bungeni ili ijadiliwe kama ilivyokuwa kwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabau za Serikali (CAG).
Alisema ripoti ya Takukuru inayo majina ya vigogo wengi waliohusika kuchota fedha za Tegeta Escrow na kwamba ikiwekwa wazi itasaidia wananchi kuwajua wahusika zaidi wa kashfa hiyo.
Akizungumzia kuhusu viongozi hao kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) waliochaguliwa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, alisema safari ndiyo imeanza kinachofatia ni kuwahimiza wananchi wengine kujiunga na Ukawa ili kuweza kuing’oa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika chaguzi zinazokuja ukiwamo wa madiwani, wabunge na urais.
Alitaka wanafunzi wa vyuo vikuu vyote vilivyopo katika mkoa wa Morogoro ambao ni wanachama wa Ukawa kutumia muda wao wa siku za mapunziko kuingia mitaani na vijiweni kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kujiunga kujiunga na Ukawa ili kuiondoa CCM madarakani.
KAULI YA BUNGE
Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, alithibitisha Kafulila kuwasilisha kusudio la kuomba awasilishe hoja binafsi katika mkutano ujao wa Bunge, lakini hajaruhusiwa.
Dk. Kashilila alisema baada ya kuwasilisha kusudio hilo, ofisi ya Spika imemtaka Kafulila awasilishe maelezo ya hoja yake ili kuona kama ina maelezo gani kabla ya kumruhusu kuiwasilisha bungeni.
“Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, mbunge akishawasilisha kusudio anaandikiwa barua ya kutakiwa awasilishe maelezo ya hoja yake kuona kama hayapingani na kanuni za bunge, hadi sasa Kafulila bado hajawasilisha maelezo,” alisema.
LEMA, NASSARI KUWASHA MOTO BUNGENI
Katika hatua nyingine, wabunge wawili wa mkoa wa Arusha, wametangaza rasmi kuwa watakuwa wa kwanza kufukuzwa bungeni na Spika, Anne Makinda, iwapo Prof. Muhongo hatakuwa amewajibishwa ama kujiuzulu mwenyewe.
Hatua ya wabunge hao ambao ni Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, kutoa kauli hiyo kunatokana na kutowajibishwa kwa Prof. Muhongo hadi sasa licha ya wabunge katika mkutano wa 16 na 17 kutoa maazimio ya kutaka watuhumiwa wa sakala la uchotwaji fedha zaidi ya Sh. bilioni 300 za akaunti ya Tegeta Escrow wawajibishwe akiwamo waziri huyo.
Lema (Chadema) akizungumza na wananchi wa manispaa ya Moshi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Penfold, alisema atakuwa mbunge wa kwanza kufukuzwa na Spika Makinda katika kikao cha 18 cha bunge kijalo iwapo Prof. Mhongo, atakuwa hajawajibishwa.
“Ndugu zangu, ninawaambia kabisa kwamba katika mkutano ujao wa Bunge, kutawaka moto, nikikuta Prof. Mhongo bado ni Waziri wa Nishati na Madini, kwamba hajawajibisha na mamlaka ya uteuzi au kujiuzulu mwenyewe, nitakuwa mbunge wa kwanza kufukuzwa,” alisema Lema.
alisema atakapowajibishwa Prof. Muhongo hatua itakayofuata ni kupambana na Serikali ili iboreshe daftari la kudumu la wapigakura na hiyo ndio itakuwa safari ya mwisho kisiasa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa upande wake, Nassari (Chadema), alimuunga mkono Lema, akisema atakuwa mbunge wa pili kufukuzwa ndani ya bunge hilo kama Prof. Muhongo atakuwa hajawajibishwa.
“Kama maazimio ya mkutano wa Bunge wa 16 na 17 mwaka jana, hayajatekelezwa kwa ukamilifu ikiwamo Muhongo kuwajibishwa na kama ilivyofanywa kwa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, atakayefuatia kufukuzwa bungeni baada ya Lema ni mimi kwa sababu simnaujua muziki wangu?” alihoji na kuongeza: “Lazima Muhongo ang’ooke.”
Novemba mwaka jana wakati wa kikao cha 16 na 17, Bunge liliazimia kwamba katika sakata la akaunti ya Tegeta Escrow wahusika wote wawajibishwe.
Waliotakiwa kuwajibishwa na ni Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco); Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka na Waziri Muhongo, ambao walitakiwa kuwajibishwa na mamlaka ya uteuzi.
Wengine ni wenyeviti wa Kamati tatu za Bunge hilo, Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na Andrew Chenge (Bajeti).
Bunge lilishauri kuwa hatua za haraka zichukuliwe na Kamati husika za Bunge kabla ya kuanza kwa mkutano wa 18 wa Bunge.
Hadi sasa aliyefukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete ni Prof. Tibaijuka na huku Jaji Werema akijiuzulu.
Maswi alisimamishwa kazi na Katibu Mkuu, Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
WALIOFIKISHWA KORTINI
Hadi sasa watumishi watano wa serikali wamefikishwa kizimbani kwa tuhuma za kupokea mgawo wa fedha za Escrow.
Vigogo wa kwanza kufikishwa mahakamani jumatano iliyoputa ni Teophil John, Mhandisi Mwandamizi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Teophil walifikishwa mahakamani kwa kudai kudai na kupokea rushwa kutoka kwa James Rugemalira, Jumatano iliyopita.
Ijumaa iliyopita Mkurugenzi wa Fedha wa Benki Kuu (BoT), Julius Angello; Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven Urassa na Meneja wa Misamaha ya Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kyabukoba Mutabingwa nao walifikishwa mahakamani.
Imeandikwa na Ashton Balaigwa, Morogoro; Godfrey Mushi, Rajabu Mmbughu, Moshi na Thobias Mwanakatwe, Dar. CHANZO: NIPASHE
UKAWA KUKOMAA NA PROF MUHONGO, TIBAIJUKA NA WEREMA, WATAKA WAFIKISHWE KORTINI.
Reviewed by habari motto
on
1:36 PM
Rating: