Ndugu
na majirani pamoja na watu waliohudhuria mazishi wakiwa katika Ibada
kabla ya kwenda makaburini , Malamba mawili jijini Dar es Salaam jana
kwa ajili ya mazishi.
Mapya
yameibuka katika mauaji ya Farahan Maluli (30), anayedaiwa kuuawa na
rafiki yake ambaye ni mtoto wa bosi wake baada ya ndugu wa marehemu
kuzungumzia jinsi marehemu alivyokuwa akitoa fedha kwa mtuhumiwa wa
mauaji hayo.
Ndugu
wa marehemu walifichua siri hiyo wakati wakizungumza na paparazi
kwenye mazishi ya kijana huyo yaliyofanyika jana eneo la Malamba Mawili
Mbezi Mwisho, jijini Dar es Salaam.
Kaka
wa marehemu, Abdallah Yusuf, alisema Farahani (marehemu), kabla ya
mauti hayo kumkuta, alikuwa akitoa fedha kwa awamu kwa ajili ya
kununulia gari la kusombea mchanga ‘tiper’ kwa bei ya Sh. milioni 35.
Alisema
katika makubaliano hayo, Farahani alianza kutoa Sh. milioni 17, mara ya
pili milioni 10, mara ya tatu Sh. 500,000 na baadaye akamalizia kwa
kutoa Sh. 2,500,000 ambazo alimkabidhi rafiki yake na mtuhumiwa siku
moja kabla ya mauti kumkuta.
Alisema mdogo wake alipotea Juni 11, mwaka jana na taarifa zilitolewa katika Kituo cha Polisi Mbezi kwa Yusuf.
Abdallah
alisema baada ya uchunguzi kufanyika, polisi walifanikiwa kumkamata
mtuhumiwa ambaye ni Hemed Hamis na kumuweka kituoni kwa muda wa wiki
mbili kabla ya kutolewa nje kwa dhamana kwa madai alikuwa mgonjwa.
“Mdogo
wangu alivyopotea nilikuwa natumiwa meseji kupitia simu yake ambazo
zilikuwa zinasema `mdogo wako huwezi kumpata hadi pale utakapokuja
kunikabidhi fedha zangu Shilingi milioni 75 ,” alisema.
Alisema
simu hiyo iliendelea kutumiwa kwa mwezi mmoja na baada ya hapo
haikupatikana tena, kitendo kilichowafanya ndugu kukutana kujadili suala
hilo na baadaye walikata tamaa.
“Tulikata
tamaa kumtafuta baada ya kumtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio na pia
simu tulizokuwa tunapigiwa zilikuwa hazipatikani tena,” alisema na
kuongeza:
“Pia
simu za vitisho zilitupa wasiwasi na kudhani mdogo wetu alishiriki
vitendo viovu ambavyo vilitufanya tuamini kuwa mdogo wetu ametoroka
kwenda nje.”
Naye
dada wa marehemu ambaye hakutaka jina lake liandikwe mtandaoni, alisema
Jumatatu wiki hii, walipigiwa simu na polisi wa Kituo cha Polisi Mbezi
kwa Yusuf na kuwataka waende Kituo cha Polisi Msimbazi.
Alisema
baadaye kaka yao ambaye ni Abdallah, aliporudi kutoka Kituo cha Polisi
Msimbazi, aliwaeleza kuwa Faharani (marehemu), aliuawa na rafiki yake
Hemed na alimfukia kwenye nyumba aliyokuwa anaishi.
Aliongeza
kuwa polisi waliwachukua ndugu zao wa kiume na kwenda nao katika nyumba
aliyokuwa akiishi mtuhumiwa (Hemed) iliyopo eneo la Ilala Sharif
Shamba, jijini Dar es Salaam.
Alisema
walipofika katika nyumba hiyo, walionyeshwa eneo ambako Farahani
alikuwa amezikwa na kuanza kuufukua mwili wake na kuuchukua kwenda nao
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi.
Hata
hivyo, zoezi la kufukua mwili huo lilikuwa na changamoto kutokana na
mtuhumiwa kuonyesha eneo la uani ambalo halikuwa lenyewe.
Jirani
mmoja ambaye alikuwapo eneo la tukio, aliwaonyesha polisi eneo ambalo
alikuwa na shaka nalo na ndipo polisi walipoanza kufukua mwili huo.
Taarifa
zinaeleza kuwa kazi ya kufukua mwili wa marehemu huo ulianza saa 4:00
asuhubi na kumalizika saa 8:00 kutokana na shimo alilokuwa amezikwa kuwa
na urefu wa mita 10.
Naye
Mustapha Mwalongo, aliyekuwa akifanya kazi na marehemu, alisema
alimfahamu Farahani kuwa mfanyakazi wa mabasi ya kampuni ya Noraz na
Waheed.
Alisema alimuamini Hemed kwani alikuwa ni mtoto wa bosi wake na aliyekuwa karibu naye.
Mwalongo
ambaye pia ni Mjumbe wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa),
alisema kufuatia marehemu kumdai sana mtuhumiwa, ilifikia hatua
akamweleza baba yake na mtuhumiwa, hali iliyosababisha urafiki wao
kuvunjika.
Kwa
upande wake, rafiki wa karibu wa marehemu, Somji Nawanda, alisema Hemed
(mtuhumiwa), alimpigia simu marehemu Juni 9, mwaka jana na kumtaka
aende Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kulipia ushuru wa
gari alilomwagiza.
Alisema
alipofika TRA, walimtafuta Hemed ambaye alidai kuwa muda huo alikuwa
Kariakoo na baadaye alimpigia simu na kumwambia aonane na mtu mmoja
aitwaye Said amkabidhi Sh. milioni 2.5.
“Marehemu
alisita, lakini Hemed alimwambia ni pesa ngapi umenipa unashindwa
kuniamini kwa fedha hizo? Ndipo marehemu alipomkabidhi fedha hizo Said
na kumwambia asubiri aingie TRA amchukulie stakabadhi, aliporudi Said
alisema mtandao unasumbua hivyo hawezi kupata stakabadhi waonane naye
tena Juni 11, mwaka jana kwa ajili ya kuchukua gari,” alisema Nawanda.
Mmoja
wa majirani aliyejitambulisha kuwa ni Mama Salum, alisema hawakuwa na
taarifa kama jirani yao alifariki dunia kutokana na kazi zake za uwakala
ila walidhani amesafiri.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki, alipotafutwa juzi kwa njia ya
simu, alisema alikuwa barabarani akiendesha gari na kuahidi kuwa
akishuka atapiga simu.
Hata hivyo, baada ya kuendelea kupigiwa simu, alituma ujumbe mfupi (sms) akisema kuwa angepiga muda mfupi, ingawa hakupiga.
Hata alipopigiwa na kutumiwa sms, hakupokea hadi tunakwenda mitamboni.
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipopigiwa
awali, alielekeza apigiwe Nzuki, akisema kuwa ndiye mwenye taarifa hizo.
Jumatatu
wiki hii, polisi, ndugu na wakazi wa Ilala Sharif Shamba, jijini Dar es
Salaam, walifichua kuuawa kwa Farahani aliyeuawa na rafiki yake kisha
kumfukia kwenye shimo alilochimba na kulifukia pamoja na kulisakafia
uani kwenye nyumba aliyokuwa akiishi mtuhumiwa.
Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa Julai, mwaka jana, baada ya mtuhumiwa kudaiwa kushindwa kumlipa rafiki yake huyo Sh. milioni 35.
Mauaji Ya Mteja Wa Gari, Ndugu Wasimulia
Reviewed by habari motto
on
11:30 AM
Rating: