Taarifa Sahihi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kuhusu Kifo cha Askari Wake Huko Mbalizi


Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania linapenda kutoa taarifa ya kifo cha Askari wake Praiveti Ahadi Mwaka Mwainyokole kilichotokea tarehe 4 Februari 2015 katika mji mdogo wa Mbalizi, Mkoani Mbeya.

Taarifa za mazingira ya kifo cha Askari huyo zimepotoshwa na baadhi ya Vyombo vya Habari na kusababisha mapokeo tofauti kwa wananchi.

Hali halisi ni kwamba, mnamo tarehe 4 Februari 2015 Askari huyo akiwa na Askari wenzake wanne (4) ambao ni Koplo Bedatu Benard Mloka, Praiveti Thani Hamisi Haji, Praiveti Mzee Buan Mzee na Praiveti Mohamed Juma walivamiwa na kundi la wahuni wakati wakitoka matembezini. Chanzo cha vurugu hizo ni kutokana na Praiveti Rashid Maulid wa Kikosi chao kuibiwa samani kwenye nyumba aliyokuwa amepanga uraiani katika mji mdogo wa Mbalizi, Kitongoji cha Shigamba. Samani alizoibiwa ni pamoja na TV aina ya LG “flat screen” “Inch 20”, radio aina ya Sony moja, Deck aina ya Sangsung, flash moja, extension cable moja na fedha taslimu Tshs 30,000/=.

Askari huyo alitoa taarifa Kituo cha Polisi tarehe 03 Februari 2015 na kupatiwa RB yenye Nambari MBI/RB/285/2015, sambamba na kutoa taarifa Polisi. Kituo hicho cha Polisi kilitoa askari mmoja ambae aliungana na askari Jeshi na wenzake na wakaenda eneo la relini ambako vijana wasio na ajira maalumu hushinda. Waliwakamata vijana saba, mmoja wa vijana hao alikimbia na kwenda kuwapa taarifa wenzao ambao hawakuwepo katika eneo hilo ambapo vijana sita walifikishwa kituo cha Polisi.

Ilipofika saa tatu usiku askari hao wakiwa katika matembezi ya kawaida walikutana na kundi la vijana wakiwa na silaha mbalimbali kama nondo na marungu ambao walianza kuwashambulia huku wakiwashutumu kuwa waliwapeleka wenzao Polisi.

Kwa kuwa kundi la vijana hao lilikuwa kubwa na likiwa na silaha zilizotajwa lilifanikiwa kuwajeruhiAskari hao akiwemo Praiveti Ahadi Mwainyokole ambae alijeruhiwa vibaya.
Askari hao walikwenda Polisi na wakachukuwa PF3 na kisha kwenda katika hospitali ya Jeshi Mbeya baadaye Praiveti Mwainyokole alifariki muda mfupi baada ya hali yake kutokuwa nzuri kutokana na kupigwa na kitu kizito kichwani hali iliyosababisha damu kuvia kwenye Ubongo.

JWTZ linasikitishwa na mauaji hayo yaliyofanywa kwa Askari wake, na mauaji ya askari wengine katika maeneo ambako vitendo kama hivyo vimetokea. Ikumbukwe kuwa JWTZ lipo kwa ajili ya usalama na ustawi wa wananchi, hivyo JWTZ linalaani vitendo viovu vinavyofanyika kwa askari wake na linatoa rai kwa vyombo vya sheria kuchukua mkondo wake.

Kimsingi JWTZ halina ugomvi na wananchi kwani kazi yake ya msingi ni kuwalinda ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kimaendeleo kwa utulivu na amani kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu.

Imetolewa na
 Kurugenzi ya Habari na Mahusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
 Loans                                    
Taarifa Sahihi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kuhusu Kifo cha Askari Wake Huko Mbalizi Taarifa Sahihi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kuhusu Kifo cha Askari Wake Huko Mbalizi Reviewed by habari motto on 3:06 PM Rating: 5
ads 728x90 B
Powered by Blogger.