Akihojiwa katika kipindi Clouds 360 kinachorushwa na Televisheni cha Clouds aliulizwa maswali ambayo baadhi hakuyatolea majibu.
Baadhi ya swali lililoulizwa na msikilizaji wa kipindi hicho, aliyetaka kujua kama aliyemtishia bastola, Nape Nnauye alikamatwa au hakukamatwa.
Mwigulu alisema wanachofahamu aliyemtishia risasi Nape hakuwa polisi kama ambavyo ilidhaniwa. Lakini hakusema kama siyo polisi alikuwa ni nani.
Alisema katika tukio kama lile wahalifu wanaweza kutumia nafasi hiyo kufanya waliyoyafanya.
Hata hivyo, Mwigulu alisema uchunguzi wa suala hilo bado unaendelea.
Kuhusu Ben Saanane, Mwigulu aliulizwa kama alikufa au bado yuko hai akajibu kuwa Serikali haijui kama Ben Saanane alikufa au yuko hai lakini Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta ili kuujua ukweli.
Saanane ambaye alikuwa Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti wa Chadema na Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitoweka tangu Novemba 2016.
“Ni ngumu kusema kama Ben Saanane yuko hai au amefariki kwa sababu bado hatujui nini kilimpata,” alisema.
Alisema Polisi bado wanaendelea kumtafuta na akataka watu wenye taarifa zinazoweza kusaidia kupatikana kwake wafanye hivyo kwa kuwapa taarifa polisi.
“Msidhani kwamba Serikali haifanyi chochote, suala ambalo linahusisha maisha ya mtu hatupuuzi hata kidogo tunaendelea na upelelezi,” alisema.
Kuhusu Lissu kutoa taarifa kwamba kulikuwa na gari lililokuwa likimfuatilia katika eneo la Oysterbay jijini Dar es Salaam siku chache kabla ya kushambuliwa kwa risasi, Mwigulu alisema aliliagiza Jeshi la Polisi kufuatilia.
“Lakini baada ya kuchunguza tulikuta gari lenye namba ambazo Lissu alidai lilikuwa likimfuatilia likiwa Arusha na halijawahi kuwa Dar es Salaam,” alisema.
Akifafanua, Mwigulu alisema alimuona Lissu siku ya tukio Septemba 7 akiwa katika Hospitali ya Rufaa Dodoma na baadaye uwanja wa ndege aliposafirishwa kwa ajili ya matibabu jijini Nairobi nchini Kenya ambako yuko hivi sasa.
Alipoulizwa kwa nini yeye kama waziri hajaenda kumwona Lissu Nairobi, alijibu kuwa yeye wananchi wenzake wa Mkoa wa Singida wana utaratibu wamejiwekea wa kuwakilishwa na Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu.
“Katika mazingira mengine kama Serikali tunaendelea kupata taarifa za Lissu kupitia balozi aliye huko,” alisema.
Lissu akipona atatusaidia upelelezi
Akimzungumzia Lissu, Mwigulu alisema Lissu na dereva wake Simon Bakari wakipona watalisaidia Jeshi la Polisi katika upelelezi wa tukio hilo.
“Lissu tunamuombea apone haraka kwani atatoa mchango mkubwa wa kusaidia uchunguzi, mtu akiwa kwenye maumivu makali huwezi kumuuliza lolote,” alisema.
Aliongeza, “ tunaheshimu ushauri wa madaktari kwamba wote wawili wanahitaji utulivu katika kipindi hiki, wakipona watatusaidia.”
Alisema kutokana na upya wa uhalifu wa aina iliyotokea kwa Lissu, kuna mambo wanaendelea kuyafuatilia ambayo hawezi kuyaeleza kwa sasa.
“Suala la Lissu kutokana na upya wake, kuna vitu tunaendelea kuvifuatilia, hivyo kuna mambo hatuwezi kuyasemea,” alisema Aliwataka watanzania Watanzania kuendelea kuwa na subira wakati kazi ya uchunguzi ikiwa inaendelea.
Mwigulu alisema baada ya tukio la kushambuliwa Lissu Septemba 7, taarifa kadhaa zilichukuliwa eneo la tukio ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi ili kupata undani wake.
“Wahalifu hawajakamatwa wote, ukianza kusema itakuwa ni shida, kuna mambo yanaendelea kufanywa na hayana ukomo. Ukomo utafikiwa endapo wote waliohusika watakamatwa. Nikisema naweza kuvuruga kazi inayoendelea,” alisema.
Akijibu swali la mtangazaji wa kipindi hicho kuwa watu wanahoji kwamba askari wanapouawa wahalifu wanakamatwa mapema Mwigulu amesema, “ Watu wakiwaza hivyo watakuwa wanakosea, hatuweki madaraja, ni mazingira ya tukio tu ndilo linalosababisha baadhi wakamatwe haraka na wengine tuchelewe kuwakamata.”
Alisema kwa sasa hawezi kueleza ni watu wangapi wamekamatwa lakini kuna magari zaidi ya 10 yanayofanana na lililohusika kwenye tukio ambayo yamekamatwa.
Maiti zinazookotwa
Alipoulizwa kuhusu maiti zinazookotwa mara kwa mara, Waziri alisema maiti zinazookotwa zikiwa zimetelekezwa uchunguzi unaonyesha wanaofanya hivyo ni wanaosafirisha binadamu kwa njia zisizo halali.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio tofauti ya miili ya watu kukutwa ikiwa imefungwa kwenye viroba na mingine ikiwa imefungwa mawe na kutumbukizwa mtoni na baharini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema kumekuwa na watu wanaosafirisha binadamu kutoka Somalia na Ethiopia kwenda Afrika Kusini kupitia Tanzania.
“Wamekuwa wakiwatupa baharini wanapokuwa wamekufa, kuna wengine 80 walitupwa wakiwa mahututi mpakani mwa Tanga na Bagamoyo na polisi walijitahidi kuwatengenezea uji mwepesi ili kuokoa kwanza uhai wao,” alisema.
Mwigulu alisema watu hao husafirishwa kama vile mizigo kwenye malori na wanapokufa kwa kukosa hewa miili yao hutupwa.
Alisema kwa kuwa husafirishwa kwa njia haramu, wakishakufa miili yao hutupwa kwenye mito ili kukwepa kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Kumekuwa na matukio ya aina hiyo mara nyingi lakini wanaofanya biashara hiyo tumekuwa tukiwakamata na kuwafikisha mahakamani,” amesema.
CREDIT KWA mwananchi.co.tz
CREDIT KWA mwananchi.co.tz
Mwigulu awekwa kona mauaji, utekwaji unaofanyika nchini
Reviewed by habari motto
on
7:04 AM
Rating: