FUATA MBINU HIZI KURUDISHA MAPENZI KWA MPENZI WAKO



Kugombana ni jambo ambalo halikwepeki katika uhusiano wa kimapenzi. Upo ugomvi
 ambao ni wa kawaida na huisha kirahisi lakini upo ugomvi ambao huwa mkubwa na kama
 ukitokea na ukashindwa kujua nini cha kufanya kuweka mambo sawa, husababisha ufa 
kwenye penzi lenu.Leo tutazungumzia mambo muhimu ya kufanya inapotokea wewe na 
mpenzi wako mmeingia katika ugomvi mkubwa, mmetoleana maneno machafu au hata 
kupigana. 

1. TAFAKARI CHANZO CHA TATIZO
Kuna usemi kwamba ukitaka kulitatua vizuri tatizo ni lazima kwanza ujue chanzo cha tatizo
 lenyewe. Ukishindwa kugundua chanzo cha tatizo, basi na wewe unakuwa sehemu ya tatizo. 
Utashangaa kwamba wapenzi wengi hugombana na mambo kuwa makubwa kabisa kwa
sababu ya vyanzo vidogo ambavyo walishindwa kuvigundua mapema na matokeo yake vikazaa matatizo 
mengine.
Mfano rahisi, chanzo kinaweza kuwa mpenzi wako amekupigia simu lakini ukashindwa 
kuipokea kwa muda muafaka. Atakapopiga kwa mara nyingine au mkikutana, usitegemee 
atakufurahia kwa sababu atahisi umemdharau kwa kutopokea simu yake.Endapo ukifanya 
makosa ya kushindwa kuliona kosa lako mapema na kushindwa kuomba radhi au kutoa 
maelezo yanayoeleweka kwa nini hukupokea simu, matokeo yake utamjibu vibaya, naye 
atakujibu vibaya na mwisho mtaishia kupigana au kuachana kabisa mkiwa mmeshatoka
 kabisa kwenye kosa la msingi.
Bila shaka msomaji wangu umeona jinsi chanzo kidogo kinavyoweza kusababisha tatizo 
kuwa kubwa. Ndoa nyingi au uhusiano unaofika mwisho huwa umesababishwa na mambo
 madogo ambayo yalishindwa kutafutiwa suluhu mapema.
Katika kila ugomvi unaotokea, jambo la kwanza jipe muda wa kutafakari chanzo 
kilichosababisha mkagombana. Wakati mwingine wewe ndiyo unaweza kuwa chanzo cha 
tatizo lakini kama ukiyajua makosa yako mapema na kukiri kisha kuomba radhi kwa 
mwenzio, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kurudisha mapenzi kwa haraka.

2. MPE MUDA HASIRA ZIISHE
Kila binadamu ameumbwa akiwa na hasira na kwa bahati mbaya ni wachache wanaoweza 
kuzidhibiti hasira zao. Ni rahisi mtu kutukana, kupiga au kuharibu vitu akiwa na hasira.
Baada ya kugombana, kila mmoja lazima atakuwa na hasira na njia pekee inayoweza 
kuepusha matatizo zaidi, ni kujipa muda na kumpa muda mwenzako ili hasira zipungue.
Kama mpo sebuleni na umetokea ugomvi, ni busara kwenda chumbani au nje mpaka hasira 
zako zikiisha. Ni makosa kulazimisha suluhu wakati kila mmoja akiwa na jazba kwani 
mtaishia pabaya zaidi. 
Ukishaona hasira zako zimetulia na mwenzako naye ametulia, unaweza kuanzisha mada
 juu ya kilichosababisha mkagombana. Tumia lugha ya upole kwani endapo utakuwa 
ukifoka au 
kuzungumza kwa sauti ya juu, matokeo yake mtarudia tena kugombana.

3. MPE NAFASI YA KUZUNGUMZA
Huwezi kumuelewa mtu kabla hujampa nafasi ya kuzungumza na kumaliza kile 
alichokusudia kukisema. Endapo tatizo limetokea na upo kwenye hatua za kusaka suluhu, 
mpe mwenzako nafasi ya kueleza dukuduku lililopo ndani ya moyo wake.
Usimkatishe wala kumbishia 
chochote, muache aongee ulichomuudhi mpaka dukuduku lake liishe kisha na wewe jieleze
 kwa upole na sauti tulivu.

4. OMBA MSAMAHA
Hakuna silaha nzuri inayoweza kukusaidia kuushinda ugomvi wowote na kutuliza mambo 
kabla hayajawa mabaya kama kuomba msamaha. Neno ‘samahani’ ni dogo lakini lina maana 
kubwa kwa yule mtu anayelitoa na anayelipokea.
Hata kama unaona dhahiri kwamba kosa siyo lako, omba msamaha kwanza kisha baada ya
 hapo anza kumuelewesha mpenzi wako kwa upole. Lazima mwisho na yeye atayaona 
makosa yake na kukuomba msamaha, mtaweza kuepuka kuukuza ugomvi huo na 
kurudisha hisia za mapenzi.

5. USIWEKE KINYONGO
Endapo umeamua kuomba msamaha kwa mpenzi wako, au yeye amekuomba msamaha, 
samehe kwa dhati kutoka ndani ya moyo wako na sahau kile kilichotokea. Ni kosa kubwa 
kuweka kinyongo rohoni, yaani unamwambia kwamba umemsamehe wakati moyo wako 
bado una hasira naye. Ukisamehe kwa dhati, jifunze na kusahau kwani kusamehe 
kunaenda sambamba na kusahau.
Wazungu wanasema forgive and forget. Elewa kwamba mpenzi wako ni binadamu ambaye 
hajakamilika, wala si malaika.
Lazima atakuwa akikosea mara kwa mara, endapo utakuwa ukilimbikiza vinyongo, unafuga
 matatizo makubwa kwani siku nyingine akikukosea hata jambo dogo, utakumbushia na ya
 jana na juzi na mwisho ugomvi utakuwa mkubwa sana.
Kwa maoni, ushauri au swali nicheki kwa namba za hapo juu.
FUATA MBINU HIZI KURUDISHA MAPENZI KWA MPENZI WAKO  FUATA MBINU HIZI KURUDISHA MAPENZI KWA MPENZI WAKO Reviewed by habari motto on 7:49 AM Rating: 5
ads 728x90 B
Powered by Blogger.