JESHI LA ZIMA MOTO LATOA TAMKO KWA WANAFUNZI WAKE WENYE VIRUSI VYA UKIMWI

JESHI la Zimamoto na Uokoaji limedai kuwa askari wanafunzi 37 waliyofukuzwa mafunzoni katika chuo cha Magereza Kiwira, Tukuyu mkoani Mbeya ni kutokana na kutokidhi vigezo mbalimbali tofauti na inavyodaiwa kwamba wamekutwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU).
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Jeshi hilo, Inspekta Puyo Nzalayaimisi, alisema kama Jeshi wana taratibu na vigezo ambavyo mtumishi anatakiwa kukidhi na hilo suala la kwamba wana VVU halina ukweli wowote.


Akifafanua zaidi, Inspekta Nzalayaimisi, alisema hata kama ingetokea mtu akakutwa katika hali hiyo, wasingeweza kumfukuza au kumtangaza mbele ya watu kama ilivyodaiwa, kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma.


Kwa mujibu wa Msemaji huyo, ili kuhakikisha watu wenye maambukizi hawanyanyapaliwi, ndio maana katika bajeti hutenga fungu kwa ajili ya kuhudumia watu wa aina hiyo.


Hata hivyo, alisema mojawapo ya vigezo ambavyo askari anaweza kuondolewa kutokana na kutokidhi, ni pamoja na ugonjwa wa pumu au kifafa kutokana na aina yao ya kazi wanayoifanya ya moto, hairuhusu watu wa aina hiyo.


“Hebu niambie… kwa kazi yetu unaweza kumuajiri mtu ambaye anaanguka kifafa aende akazime moto, na vitu kama hivi wananchi wanapaswa kujua kwamba haviwezi kugundulika pale tunapowasaili, bali hujitokeza wakati mwingine wakiwa kwenye mafunzo,” alisema.


Habari za kufukuzwa kwa wanafunzi hao, zililifikia Tanzania Daima Septemba 2 mwaka huu, kutoka katika chanzo cha kuaminika.


Chanzo hicho kilidai kwamba, taarifa za wenzao kutimuliwa walitangaziwa majira ya saa 4:00 asubuhi baada ya kupata chai, ambazo ziliwashtua sana na kuona huo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.


Kiliongeza kuwa, cha kusikitisha zaidi ni kwamba wamebakiza wiki mbili kumalizia masomo yao japokuwa kwa taratibu za mafunzo hayo zinaeleza kuwa, huwa hawana muda maalum kwani hutolewa baada ya uongozi kuona wameiva.

>>Tanzania daima
JESHI LA ZIMA MOTO LATOA TAMKO KWA WANAFUNZI WAKE WENYE VIRUSI VYA UKIMWI JESHI LA ZIMA MOTO LATOA TAMKO KWA WANAFUNZI WAKE WENYE VIRUSI VYA UKIMWI Reviewed by habari motto on 11:43 AM Rating: 5
ads 728x90 B
Powered by Blogger.