UCHAGUZI wa serikali za mitaa huko Geita umefunguliwa kwa vurugu kubwa ambapo mkurugenzi wa siasa na uenezi wa chama cha wananchi(CUF)katika kata ya Kagu wilayani Geita Fransisco Kadimu(34)amenusurika kufa baada ya kukatwa mapanga kichwani na vidoleni na watu wanaodaiwa ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM).
Kutokana na hali hiyo wananchi wa eneo hilo walikasirishwa na kitendo hicho na kulazimika kupiga yowe kujikusanya na baadaye waliamua kuvamia makazi ya watuhumiwa kisha kuyasambaza na kuchoma moto moja ya pool table ya mtuhumiwa wa ukataji mapanga.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Desemba 14 saa 5 usiku katika kijiji cha Kinaki kata ya Nyawilimilwa Wilayani Geita Katika mkoa wa Geita.
Akizungumza kwa taabu na Dunia Kiganjani Blog akiwa katika hospitali ya Wilaya ya Geita Kadimu alidai kuwa alikumbana na wakataji hao wakati akitokea kwa katibu wa chama chake anayeishi kijijini hapo.
Alisema,akiwa ameivuka senta ndogo ya Calfonia ndipo alipokutana na watu hao ambao aliwatambua kwa majina na sura ambao bila huruma walianza kumkat akata mapanga kichwani na mikononi sambamba na kumpiga kwa fimbo na marungu hali iliyopelekea kupoteza fahamu.
Alisema,alikuja kupata fahamu baadaye na kujikuta amezungukwa na wananchi waliofika eneo hilo kufuatia mayowe aliyopiga kabla ya kuzirai na ndipo walipomkimbiza katika hospitali ya Wilaya ya Geita anakoendelea na matibabu.
Katika tukio hilo mbali na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za kichwani pia kidole chake kimoja cha mkono wa kulia kilinyofolewa kwa panga na kubakia na ulemavu.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo afisa mtendaji wa kijiji cha Nyawilimilwa Charles Kidingi alisema,baada ya tukio hilo wananchi walihamasishana na kwenda kuvunja makazi ya watuhumiwa hao pamoja na kuteketeza kwa moto pooltable la mmoja wa watuhumiwa hao.
Aliwataja watu wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo ambao ni makada wa CCM kijijini hapo kuwa ni pamoja na Mashiku Ndezu,Deo Ndezu,na wengine waliofahamika kwa jina moja la Raulian na Alex ambao wamekimbilia kusikojulikana.
Na Valence Robert - Dunia Kiganjani blog Geita
Geita Wakatana Mapanga, Kiongozi Wa CUF Afyekwa Vidole
Reviewed by habari motto
on
9:31 AM
Rating: