Licha Ya Kuiletea Nchi Heshima Diamond Nusura Achomwe Kisu

STORI: MUSA MATEJA, GLADNESS MALLYA NA HAMIDA HASSAN.
Licha ya kuiletea sifa kubwa Tanzania kwa kutwaa tuzo tatu za Channel O, mkali anayekimbiza katika anga la muziki wa Kizazi Kipya Bongo, Nasibu Abdul ‘Diamond Platinumz’ amenusurika kuchomwa kisu baada ya kushuka kwenye gari na kujichanganya na mashabiki wake.
Mkali  wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platinumz’ akisndikizwa na mashabiki wake kutoka uwanja wa ndege wa Dar es Salaam.
TUJIUNGE ILALA, DAR
Tukio hilo la kutishia usalama wa staa huyo lilijiri Mitaa ya Ilala jijini Dar, Jumanne iliyopita, wakati akirejea nyumbani kutoka Afrika Kusini ‘Sauz’ alikokuwa ameweka historia mwishoni mwa wiki iliyopita.
PICHA LILIVYOANZA
Diamond aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, mishale ya saa 8:30 mchana na kupokewa na mamia ya mashabiki wake.
‘Diamond Platinumz’akitembea kwa miguu pamoja na mashabiki wake wanaomkubali.
POLISI WAMKATAZA 
Katika tukio hilo lililoshuhudiwa na wanahabari wetu, kufuatia umati mkubwa uwanjani hapo, polisi walilazimika kumkataza Diamond kuzungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali waliofika ili kusikia neno kufuatia ushindi wake mkubwa ambao umeipeleka Tanzania katika ramani ya muziki barani Afrika.
AONDOKA UWANJANI
Alipoanza kuondoka uwanjani hapo, mashabiki hao nao waliandamana naye kuelekea mjini. 
Baada ya kuona hivyo, mwimbaji huyo wa Ngoma ya Mdogomdogo alifunua sehemu ya juu (roof) ya gari lake aina ya Toyota Prado hivyo kujitokeza, huku akiziinua juu tuzo zake tatu kwa wafuasi wake hao.
Njemba mwenye kisu aliyeshukiwa kumdhuru ‘Diamond Platinumz’ katika msafara huo.
Jamaa huyo aliendelea na msafara huo katika Barabara ya Nyerere hadi alipofika Tazara, ambako msafara huo ulikata kushoto kuelekea Buguruni.Baadaye ulikata kulia kuingia katika barabara inayoelekea Kariakoo.
Msanii huyo mwenye jina kubwa Afrika, aliamua kushuka kwenye gari na kutembea kwa miguu kuwaunga mkono mashabiki wake.
ENEO LA TUKIO
Msafara huo ambao ulisindikizwa na mamia ya watu, wakiwemo waendesha bodaboda, baiskeli, magari na watembea kwa miguu, ulipoingia katika Mitaa ya Ilala, gazeti hili lilimshuhudia njemba mmoja akitafuta upenyo ili aweze kumfikia bila mafanikio, kwani kila alipojaribu kuwapita watu, alishindwa.
Mashabiki wa ‘Diamond Platinumz’wakimsindikiza kwa miguu.
KISU CHAONEKANA
Katika harakati hizo, mtu huyo ambaye hakufahamika jina wala anakotoka, kisu chake alichokuwa amekichomeka kiunoni, kilionekana kuwa na makali tayari kwa matumizi.
Wakati umati ukizidi kuongezeka na walinzi wa msanii huyo wakiwa wanahangaika kuhakikisha usalama wa bosi wao unakuwepo, hatimaye polisi nao walibaini uwezekano wa kuwepo kwa hatari, hivyo wakalazimika kumwamuru kupanda kwenye difenda yao ili kumnusuru.
WABAYA WAKE WATAJWA
Wakati hali hiyo ikijitokeza, baadhi ya watu waliohojiwa walisema wana wasiwasi na wafuasi wa msanii mwingine nyota, Ali Kiba (Team Ali Kiba) kuwa nyuma ya tukio hilo pamoja na wale wa mpenzi wake wa zamani, Wema Isaac Sepetu.
Makamanda wa Polisi wakimchukua ‘Diamond Platinumz’kwenye 'Defenda' kwa usalama wake.
“Unajua mashabiki wa wasanii hawa ni kama wana uadui, maana hii ni zaidi ya unazi, kwa vyovyote wale wa Kiba hawajafurahishwa na mafanikio ya Diamond, kama wangepata nafasi wangeweza kumdhuru,” alisema shabiki mmoja wa muziki wa kizazi kipya, aliyejitambulisha kwa jina la Zepha.
“Usije ukashangaa hata mashabiki wa Wema nao wanaweza kuwa nyuma ya jambo hili. Mafanikio ya Diamond katika tuzo hizo ni kama msumari wa moto kwao, wanaweza kujiona kama wana mikosi, huenda ndiyo maana hapo mwanzo hakuweza kushinda tuzo zingine alizoshiriki nje ya nchi,” alisema shabiki mwingine wa muziki ambaye alikataa kujitambulisha.
NENO LA DIAMOND
Alipoulizwa Diamond hakuwa na la kusema juu ya ishu hiyo zaidi ya kuwashukuru mashabiki wake waliompokea.
“Nawashuru kwa kuendelea kunisapoti. Wameonesha wanapenda mafanikio ya msanii wao,” alisema Diamond anayedaiwa kuwa ‘klozi’ na mrembo Zari mwenye maskani yake Uganda na Sauz.
Licha Ya Kuiletea Nchi Heshima Diamond Nusura Achomwe Kisu Licha Ya Kuiletea Nchi Heshima Diamond Nusura Achomwe Kisu Reviewed by habari motto on 1:56 PM Rating: 5
ads 728x90 B
Powered by Blogger.